>Mwanzo >Soma vitabu >Tokeni Mijini >Tokeni Mijini: Sehemu ya Pili

Tokeni Mijini: Sehemu ya Pili

SEHEMU YA PILI

 

 

Kuikwepa Migogoro ya Kazi

 

Ondokeni [Mijini] Kwenda Vijijini Kwenye Uhuru

 Wakati unaharakisha sana kuja ambapo uongozi wa Vyama vya Wafanyakazi utatumia uwezo wake kuleta mateso mengi kwa watu. Tena na tena Bwana ameniagiza kwamba watu wetu watoke mijini pamoja na familia zao kwenda vijijini, ambako wanaweza kujipatia chakula chao wenyewe; kwa maana siku zijazo tatizo la kununua na kuuza litakuwa zito sana. Hivi sasa tungeanza kuyatii maagizo hayo yaliyotolewa kwetu tena na tena. Tokeni mijini kwenda kwenye maeneo ya shamba [vijijini], ambako nyumba hazijasongamana sana mahali pamoja, na ambako mtakuwa huru mbali na usumbufu utakaoletwa na wale adui zetu. ----- Letter 5, 1904.

Iepukeni Migongano Iletwayo na Vyama

 Watu wamejiunga katika mashirika yenye kusudi baya ili kumpinga Bwana wa majeshi. Mashirika hayo yenye kusudi baya yataendelea kuwapo mpaka hapo Kristo atakapoondoka mahali pake pa maombezi mbele ya kiti kile cha neema, na kuvaa mavazi yake ya kulipiza kisasi [Ufu. 19:11-16]. Mawakala [wajumbe] wa Shetani wamo katika kila mji, wanashughulika sana kuwakusanya katika vyama wale wote wanaoipinga Sheria ya Mungu [Amri Kumi]. Wale wanaodai kuwa ni watakatifu na wale wanaosema waziwazi kuwa wao ni waumini wanachagua na kusimama upande wa vyama hivyo. Huu sio wakati wa kuwa dhaifu kwa watu wa Mungu. Hatuwezi kumudu kukaa bila kukesha [kuwa macho] hata kwa dakika moja. ----- Testimonies, Gombo la 8, uk. 42. (1904).

Dhiki Itakayoletwa na Vyama vya Matajiri I Mbele Yetu

 Vyama vya Matajiri [Waajiri] vitakuwa ni njia mojawapo itakayoleta duniani wakati wa taabu ambao haujapata kuwako [kuonekana] tangu mwanzo wa dunia hii. ----- Letter 200, 1903.

Migogoro Kati ya Mashirikisho ya Matajiri na Vyama vya Wafanyakazi

 Kazi wanayopaswa kufanya watu wa Mungu ni kujiandaa kwa matukio yale ya siku zijazo, ambayo yatawajia ghafula kwa nguvu nyingi. Ulimwenguni humu mashirika makubwa sana yenye ukiritimba [yanayomiliki na kuhodhi mali nyingi] yataundwa. Watu watajifunga wenyewe kwa mikataba katika vyama mbalimbali ambavyo vitawafungia katika mazizi ya yule adui. Watu wachache watajiunga pamoja na kuishika kwa nguvu mali yote iliyopatikana katika mikondo fulani ya biashara. Vyama vya Matajiri [Waajiri] vitaundwa, na wale wote wanaokataa kujiunga na vyama hivyo watakuwa watu wanaoangaliwa kwa jicho baya sana. ----- Letter 26, 1903.

Kujiandaa kwa Tukio Hilo

 Vyama vya Matajiri na mashirikisho ya ulimwengu huu yenye kusudi baya ni mtego kwetu. Achana nayo, na kwenda mbali nayo, enyi ndugu zangu. Msishirikiane nayo kabisa. Kwa sababu kwa ajili ya vyama hivyo na mashirikisho hayo yenye kusudi baya, muda si mrefu itakuwa vigumu sana kwa taasisi zetu kutekeleza kazi zake mijini. Onyo langu ni hili: Ondokeni mijini. Msijenge hospitali zetu zo zote mijini. Waelimisheni watu wetu watoke mijini kwenda mashambani [vijijini], ambako wataweza kujipatia sehemu ndogo ya ardhi, na kujijengea makazi yao wenyewe pamoja na watoto wao....

 Migahawa yetu haina budi kuwekwa mijini; maana vinginevyo watumishi wa migahawa hiyo wasingeweza kuwafikia watu na kuwafundisha kanuni za maisha bora. Na kwa wakati huu tutakalia nyumba za mikutano [makanisa] zilizomo mijini. Lakini kabla ya muda mrefu kupita kutakuwa na vita na machafuko mijini ya aina ambayo wale watakaotamani kuihama [miji] hawataweza kufanya hivyo. Yatupasa tuwe tunajiandaa [sasa] kukabiliana na matatizo hayo. Hii ndiyo nuru niliyopewa mimi. ----- General Conference Bulletin, Aprili 6, 1903.

Kuuhifadhi Utu Wetu

 Kwa miaka mingi nimepewa nuru ya pekee kwamba hatupaswi kuweka makao makuu ya kazi yetu mijini. Misukosuko na machafuko yanayoijaza miji hiyo, hali zile zitakazoletwa na Vyama vya Wafanyakazi na migomo yao, itakuwa kizuizi kikubwa kwa kazi yetu. Watu wanajaribu kuwafunga chini ya vyama fulani wale wote wanaofanya kazi mbalimbali. Huo sio mpango wa Mungu, bali ni mpango wa mamlaka ambayo kwa vyo vyote vile tusingekubaliana nayo. Neno la Mungu linaendelea kutimia; waovu wanajifunga wenyewe katika matita matita tayari kuchomwa moto.

 Hivi sasa yatupasa kutumia uwezo wote tuliopewa [na Mungu] katika kuutoa ujumbe wa onyo la mwisho kwa ulimwengu mzima. Katika kazi hii hatuna budi kuuhifadhi utu wetu. Hatupaswi kujiunga na vyama vya siri au na vyama vya matajiri na vya wafanyakazi. Tunatakiwa kusimama huru ndani ya Mungu, daima tukiwa tunamtazama Kristo kwa maagizo yake. Kuhama kwetu kote kutoka mahali fulani kwenda mahali pengine kufanyike kwa kuzingatia umuhimu wa kazi inayotakiwa kutimizwa kwa ajili ya Mungu wetu. ----- Testimonies, Gombo la 7, uk. 84. (1902)

Kuidharau Sheria ile ya Amri Kumi

 Vyama hivyo ni mojawapo ya dalili za siku za mwisho [Yakobo 5:1-6]. Watu wanajifunga wenyewe katika matita matita tayari kuchomwa moto. Pengine hao ni washiriki wa kanisa, lakini wanapojiunga na vyama hivyo, hakuna uwezekano kwao wa kutunza amri [kumi] za Mungu; kwa maana kule kujiunga na vyama hivyo maana yake ni kuidharau kabisa Sheria ile ya Amri Kumi

 "Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako" [Luka 10:27]. Maneno hayo yanaweka jumla ya wajibu wote umpasao mwanadamu. Yana maana ya kuutoa wakf mwili wote, yaani, mwili, roho, na nafsi, kwa kazi ya Mungu. Watu wanawezaje kuyatii maneno hayo, na wakati uo huo kujifunga wenyewe kwa kiapo cha kukisaidia [chama] kile kinachowanyima uhuru wa kufanya mambo yao majirani zao? Tena, inawezekanaje kwa watu kuyatii maneno hayo, na kuyaunda mashirika yanayowadhulumu watu maskini haki zao ambazo wanastahili kupata, yakiwazuia wasinunue wala wasiuze isipokuwa kwa masharti fulani yaliyowekwa? ----- Letter 26, 1903.

Vyama Vinavyoundwa au Vile Vitakavyoundwa

 Wale wanaodai kuwa ni watoto wa Mungu kwa vyo vyote vile hawatakiwi kujifungamanisha na vyama vya wafanyakazi vinavyoundwa au vile vitakavyoundwa [baadaye]. Jambo hilo Bwana anakataza. Je! wale wanaojifunza unabii hawawezi kuona na kuelewa yale yaliyo mbele yetu? ----- Letter 201, 1902.