>Mwanzo >Soma vitabu >Tokeni Mijini >Tokeni Mijini: Sehemu ya Nane

Tokeni Mijini: Sehemu ya Nane

SURA YA NANE

 

Vituo Vyetu vya Taasisi Kuwa Mbali na Msongamano wa Watu

 

Mahali Panapofaa Kujenga Taasisi Zetu

 Agizo [lile lile] bado linazidi kutolewa, Tokeni mijini. Jengeni hospitali zenu, shule zenu, na ofisi zenu mbali na vituo vyenye watu wengi. Wengi kwa wakati huu wanaomba sana ili wapate kubakia mijini, lakini wakati utakuja, muda si mrefu kuanzia sasa, ambapo wale wote wanaotaka kuziepuka tamasha na sauti hizo za uovu watakapohama na kwenda shamba [vijijini]; kwa maana uovu na uchafu utaongezeka kwa kiwango ambacho mazingira yote ya mjini yataonekana kana kwamba yamechafuliwa. ----- Letter 26, 1907.

Kuepuka Majaribu na Ufisadi

 Wengine wameshangaa kwa nini ofisi yetu ya uchapishaji inatakiwa kuhamishwa toka Oakland kwenda Mountain View. Mungu amekuwa akiendelea kuwaita watu wake kuondoka mijini. Vijana wetu ambao wamefungamana na taasisi zetu hawapaswi kuwekwa mahali pale watakapoweza kukabiliwa na majaribu na ufisadi unaoonekana katika miji mikubwa. Mountain View pameonekana kuwa ni mahali panapofaa kwa ofisi yetu ya uchapishaji. ----- Manuscript 148, 1905.

Nyakati za Dhoruba Zi Mbele Yetu

 Janga hilo [la kuteketezwa kwa moto jengo la Review and Herald] linaweza kuleta mabadiliko dhahiri katika mambo yetu. Natumaini kwamba ndugu zetu hao watalizingatia fundisho hilo ambalo Mungu anataka kuwafundisha, na ya kwamba hawatarudia kuijenga tena nyumba ya uchapishaji pale Battle Creek. Mungu anamaanisha kwamba sisi hatutakaa mijini; maana zinakuja nyakati za dhoruba kali sana mbele yetu. ----- Letter 2, 1903.

Mahali Wanapoweza Kufundishwa Kwa Ufanisi Vijana Wetu

 Mungu ametuma kwetu onyo baada ya onyo ya kwamba shule zetu na nyumba zetu za uchapishaji pamoja na hospitali zetu hazina budi kujengwa nje ya mji, mahali wanapoweza kufundishwa kwa ufanisi vijana wetu kuhusu kweli ni nini. Asiwepo mtu ye yote anayezitumia Shuhuda [zangu] kutetea ujenzi wa shughuli zetu kubwa za kibiashara mijini. Msiitangue nuru iliyokwisha kutolewa kwetu juu ya somo hilo.

 Watu watainuka [watatokea] wakisema mapotovu, wakifanya kazi yao kupinga mambo yale yale ambayo Bwana anawaongoza watumishi wake kufanya. Lakini wakati umewadia kwa wanaume na wanawake kufikiri kwa kulinganisha chanzo cha jambo na matokeo yake. Tumechelewa mno, tumechelewa mno kuanzisha mashirika makubwa ya biashara mijini ----- tumechelewa mno kuwaita vijana wetu wa kiume na wa kike watoke vijijini kuja mjini. Hali zinaendelea kujitokeza mijini zitakazofanya iwe vigumu sana kwa wale wa imani yetu kuendelea kubaki humo. Kwa hiyo, lingekuwa kosa kubwa sana kuweka fedha zetu katika ujenzi wa shughuli za kibiashara mijini. ----- Manuscript 76, 1905.

Kuishughulikia Miji Kutoka Katika Vituo Vya Mbali

 Kwa kadiri inavyowezekana, taasisi zetu zingejengwa mbali na miji. Hatuna budi kuwa na watenda kazi kwa taasisi hizo, na iwapo zinajengwa mjini, hiyo humaanisha kwamba watu wetu hawana budi kukaa karibu nazo. Lakini si mapenzi ya Mungu kwamba watu wake wakae mijini ambamo mna ghasia nyingi [makelele] na machafuko. Watoto wao na waepushwe na hali hiyo; maana mfumo mzima wa mwili huathirika kitabia kwa ghasia za kwenda huku na huko, kukimbia-kimbia ovyo na makelele. Bwana anawataka watu wake wahamie kule shamba [vijijini], ambako watakaa kwenye mashamba yao, na kupanda matunda yao pamoja na mboga za majani, tena, mahali pale watoto wao wanapoweza kuangalia moja kwa moja kazi za Mungu katika maumbile [viumbe vya asili]. Nendeni na familia zenu mbali na miji ndio ujumbe wangu.

 Kweli ni lazima isemwe, haidhuru kama watu wataisikia [wataizingatia], au wataikataa. Miji imejaa majaribu mengi. Tungepanga mipango yetu ya kazi, kwa kadiri iwezekanavyo, kwa namna ambayo tutaweza kuwazuia vijana wetu wakubwa mbali na uchafu huo.

 Miji inatakiwa kushughulikiwa kutokea kwenye vituo vya mbali. Akasema yule mjumbe wa Mungu, "Je! hivi miji hiyo haitapewa onyo? Naam; si kwa njia ya watu wa Mungu kuishi humo, bali kwa njia ya wao kuitembelea, na kuwaonya juu ya kile kinachokuja juu ya ulimwengu huu." ----- Letter 182, 1902.

Mahali Pale Ambapo Ni Rahisi Kuifikia Miji Hiyo

 Hebu watu wenye akili timamu wachaguliwe, sio kwa kusudi la kutangaza kile wanachokusudia kufanya, bali kwa ajili ya kutafuta mali ya kumiliki katika maeneo yale yaliyo katika wilaya za vijijini, mahali pale ambapo ni rahisi kuifikia miji hiyo, panapofaa kujenga shule yetu ya mafunzo kwa ajili ya watenda kazi wetu, mahali ambapo panaweza kujengwa huduma za kuwatibu watu na kuwahudumia wale wasioijua kweli. Tafuteni mahali kama hapo nje tu ya miji mikubwa, mahali ambapo majengo yanayofaa yanaweza kupatikana, aidha kama zawadi toka kwa wenye majengo hayo, au kwa kuyanunua kwa bei nzuri kutokana na misaada ya fedha iliyotolewa kwa hiari toka kwa watu wetu. Msijenge majengo katika miji hiyo iliyojaa makelele mengi. ----- Medical Ministry, uk. 308,309. (1909).

Mafundisho Toka Kwa Henoko na Lutu

 Sisi kama watu wake Mungu wanaozishika amri zake [kumi] ni lazima kuihama miji. Kama vile alivyofanya Henoko, hatuna budi kufanya kazi yetu [ya kuongoa roho] mijini, lakini tusikae humo. ----- Evangelism, uk. 78,79. (1899)

 Maovu yanapozidi sana katika taifa lo lote lile, daima husikika sauti fulani inayotoa onyo na mafundisho, kama vile sauti ya Lutu ilivyosikika kule Sodoma. Hata hivyo, Lutu angeweza kuiokoa familia yake kutokana na maovu yale mengi, kama asingalikuwa amefanya makazi yake katika mji ule mwovu, ambao ulikuwa umejaa uchafu mwingi. Mambo yote ambayo Lutu na familia yake walifanya mle Sodoma wangeweza kuyafanya hata kama wangeishi mahali fulani mbali kidogo na mji ule. Henoko alitembea na Mungu, lakini hakukaa katikati ya mji wo wote uliochafuka kutokana na kila namna ya vitendo vya kikatili vya kutumia nguvu pamoja na uovu, kama Lutu alivyofanya kule Sodoma. ----- Evangelism, uk. 79. (1903)

Makanisa, Ila Sio Taasisi, Kuwamo Mijini

 Tena na tena Bwana ametuagiza sisi kuwa inatupasa kuishughulikia miji kutokea kwenye vituo vyetu vilivyo mbali. Katika miji hiyo hatuna budi kuwa na nyumba zetu za ibada [makanisa], kama kumbukumbu za Bwana, lakini taasisi za kuchapisha vitabu vyetu, za kuponya wagonjwa, na zile za kuwafundisha watenda kazi wetu; zinapaswa kujengwa nje ya miji. Hasa ni muhimu kwamba vijana wetu waepushwe na majaribu ya maisha ya mjini.

 Inapatana na agizo hilo, kwamba nyumba za kukutania [makanisa] zimenunuliwa na kuwekwa wakf katika mji wa Washington na Nashville, ambapo nyumba za uchapishaji na hospitali zilizo katika vituo hivyo zimejengwa mbali na sehemu za katikati za miji hiyo yenye msongamano wa watu wengi sana, kama vituo vya kazi vilivyo mbali na mji. Huo ndio mpango uliofuatwa katika kuziondoa nyumba nyingine za uchapishaji pamoja na hospitali na kuzijenga mashambani [vijijini], na jambo hilo linafuatwa kule Uingereza kwa habari ya nyumba ya uchapishaji ya London pamoja na shule ya mafunzo iliyopo pale. Hivi sasa tumepewa nafasi ya kusonga mbele kwa maongozi ya Mungu yaliyofunuliwa kwa njia ya kuwasaidia ndugu zetu katika vituo hivyo muhimu na vinginevyo kwa kuanzisha kazi yetu juu ya msingi ulio imara, ili ipate kuendelezwa mbele kwa uthabiti. ----- Special Testimonies, Series B, No. 8, uk. 7,8. (1907)

 Tunatakiwa kuwa na busara kama nyoka na wapole kama hua katika juhudi zetu za kutafuta mali ya kumiliki kule shamba [vijijini] kwa bei ya chini, na kutoka kwenye vituo hivyo vya mbali tunapaswa kuihudumia miji hiyo. ----- Special Testimonies, Series B, No. 14, uk. 7. (1902)

Ujumbe Tuliopewa na Bwana

 "Tokeni mijini; tokeni mijini!" ----- huo ndio ujumbe alionipa Bwana. Matetemeko ya nchi yanakuja; mafuriko yanakuja; sisi hatutakiwi kujijenga katika miji hiyo miovu, ambamo yule adui [Shetani] anatumikiwa kwa kila njia, na ambamo Mungu mara nyingi anasahauliwa. Mungu anataka tuwe na macho safi ya kiroho. Yatupasa kuwa wepesi kutambua hatari kubwa ambayo ingeweza kuambatana na ujenzi wa taasisi zetu katika miji hiyo miovu. Yatupasa kupanga mipango yetu kwa busara ili kuionya miji hiyo, na wakati uo huo kuishi mahali pale tunapoweza kuwakinga watoto wetu pamoja na sisi wenyewe dhidi ya mivuto ile michafu inayoharibu tabia ambayo imeenea sana mahali hapo. ----- Life Sketches, uk. 409, 410. (1906)