>Mwanzo >Soma vitabu >Kristo na haki yake >Watumwa na watu huru

Watumwa na watu huru

WATUMWA NA WATU HURU

     Uwezo wa imani kuleta ushindi unaweza kuonyeshwa kwa aina nyingine ya mfululizo wa mafungu ya Maandiko, ambayo ni  ya  manufaa sana kwetu.  Kwanza kabisa, ieleweke ya kwamba mwenye dhambi ni mtumwa.  Kristo alisema:  "Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi."  Yohana 8:34.  Pia Paulo, akijiweka mahali pa mtu ambaye hajazaliwa upya, anasema:  "Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni;  bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi."  Rum.7:l4.  Mtu aliyeuzwa chini ya dhambi ni mtumwa wa dhambi.  Petro anatuonyesha jambo lilo hilo, anapozungumza  juu ya walimu waovu, wa uongo, anasema:  "Wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu, maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule." 2 Petro 2:l9.

     Tabia inayojitokeza sana ya mtumwa ni kwamba hawezi kufanya kama anavyotaka,  lakini anafungwa kufanya mapenzi ya mtu mwingine, haidhuru yawe ya kuchukiza jinsi gani.  Hivyo Paulo anauthibitisha ukweli wa usemi wake kwamba yeye, kama mtu wa mwilini, alikuwa mtumwa wa dhambi:  "Maana sijui nifanyalo;  kwa sababu lile nilipendalo, silitendi;  bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda."  "Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.  Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu , (yaani, ndani ya mwili wangu,) halikai neno jema;  kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati.  Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi;  bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo."  Rum. 7:l5, l7-l9.

     Wewe unayaita haya kuwa ni maisha ya Kikristo kweli?  Kuna wengine wanaofikiri kuwa ni ya kweli.  Basi, kwa nini mtume, kwa uchungu wa roho yake, alilia kwa kelele, "Ole wangu, maskini mimi!  ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?  Rum.7:24.  Je, hivi  Mkristo wa kweli anaweza kupitia uzoefu wa mwili wa dhambi unaotisha sana kiasi cha roho yake kulazimika kulia ili iokolewe?  La, hasha.

     Tena, ni nani yule, akijibu ombi hilo la dhati, anayejidhihirisha mwenyewe kama mkombozi?  Asema mtume, "Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu."  Katika sehemu nyingine asema hivi juu ya Kristo:-

     "Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili,  Yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo,  ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa."  Ebr.2:l4,l5.

     Tena, Kristo anatangaza utume wake Mwenyewe:

     "Roho ya BWANA i juu yangu;  kwa sababu  BWANA amenitia mafuta, niwahubiri  wanyenyekevu habari njema;  amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia  mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao."  Isa.6l:l.

     Utumwa huu na kifungo hiki kilivyo, tayari tumeonyeshwa.  Ni utumwa ule wa dhambi ----  utumwa wa kulazimishwa kufanya dhambi,  hata kama ni  kinyume na mapenzi  ya mtu  huyo, kwa nguvu iliyo ndani yetu ya uchu ule wa kutaka kufanya maovu, ambayo sisi tumeirithi ama tumejifunza kwa kuifanyia mazoezi pamoja na mazoea yetu mabaya.   Hivi Kristo anaokoa kutoka katika maisha ya Kikristo ya kweli?  La, hasha.  Kwa hiyo, utumwa ule wa dhambi, ambao mtume anaulalamikia katika sura ya saba ya Warumi, sio ule wa maisha ya mtoto wa Mungu, bali ni ule wa maisha ya mtumwa wa dhambi.  Ni kwa ajili ya kuwakomboa watu kutoka katika kifungo hiki Kristo  akaja;  si kwa kutukomboa sisi, katika maisha haya ya sasa, tusipigane vita dhidi ya dhambi na kujitahidi kushinda, bali kutoka katika kushindwa kwetu;  kutuwezesha kuwa na nguvu katika Bwana na katika uweza wa nguvu Yake, ili tupate kutoa shukrani kwa Baba ambaye "alituokoa katika  nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake,"  ambaye katika damu yake tunao huo ukombozi.

     Ukombozi huu unakujaje?  ----  Kwa njia ya Mwana wa Mungu.  Asema Kristo:  "Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru."   "Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli."  Yohana 8:3l, 32,36.  Uhuru huu unakuja kwa kila mmoja aaminiye;  maana kwa wale waliaminio jina lake, anawapa "uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu."    Uhuru kutokana na lawama unakuja kwa wale walio katika Kristo Yesu (Rum.8:l);  nasi  tunamvaa Kristo kwa imani (Gal.3:26,27).  Ni kwa njia ya imani Kristo anakaa mioyoni mwetu.