>Mwanzo >Soma vitabu >Kristo na haki yake >Ushindi wa Imani

Ushindi wa Imani

USHINDI WA IMANI

      Biblia inasema kwamba "Mwenye haki ataishi kwa imani."  Haki ya Mungu  "inadhihirishwa ... toka imani hata imani."  Rum.l:l7.  Hakuna kitu kingine cho  chote  kinachoweza kueleza vizuri zaidi jinsi imani inavyofanya kazi kuliko  baadhi ya mifano iliyoandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi, "ili kwa saburi na faraja ya Maandiko tupate kuwa na tumaini."  Rum.l5:4.  Kwanza, tutalichukua tukio maarufu ambalo  limeandikwa katika  Kitabu cha Pili cha Mambo ya Nyakati.  Hebu msomaji na afuatilie maelezo yanayofuatana kuanzia hapa katika Biblia yake.

     "Ikawa baadaye, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, na pamoja nao baadhi ya  Wameuni [Waamoni],  wakaja juu ya Yehoshafati vitani.  Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati, wakisema,  Wanakuja jamii kubwa juu yako watokao  Shamu toka ng'ambo ya bahari;  na tazama, wako katika Hasason-tamari (ndio En-gedi)."  Fungu la l,2.

     Jeshi hili kubwa lilimfanya mfalme na watu kuogopa, lakini walichukua njia ya busara kwa kukusanyika pamoja, "ili wamtafute  BWANA;  hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta  BWANA."  Fungu la 3,4.  Kisha inafuata sala ya Yehoshafati, kama Kiongozi wa kusanyiko hilo, nayo yastahili kufanyiwa utafiti  maalum, kwa vile ilikuwa sala ya imani, na ndani yake ilikuwa na chimbuko la ushindi:-

     "Yehoshafati  akasimama kati ya kusanyiko la Yuda na Yerusalemu, nyumbani mwa  BWANA, mbele  ya ua mpya;  akasema,  Ee BWANA,  Mungu  wa baba zetu,  si wewe uliye Mungu mbinguni?  tena si wewe utawalaye falme zote za mataifa?  na mkononi mwako mna uweza na nguvu, asiweze mtu ye yote kusimama kinyume chako.  Fungu la 5,6.

     Huo ulikuwa mwanzo  mzuri sana wa sala.  Inaanza na kumtambua Mungu wa mbinguni.  Kwa sababu hiyo sala  kielelezo inaanza hivi:  "Baba yetu uliye mbinguni."  Hii inaashiria nini?  ----  Kwamba Mungu, kama Mungu aliye mbinguni, ndiye Muumbaji.  Inaendeleza  utambuzi wa uweza Wake juu ya falme zote za dunia na juu ya nguvu za giza;  ukweli kwamba Yeye yuko mbinguni, ndiye Muumbaji, hudhihirisha kuwa mkononi mwake mna  uweza na nguvu, hata hakuna mtu ye yote awezaye kusimama kinyume Chake.  Kumbe!  mtu yule anayeweza kuanza sala yake wakati wa shida akiutambua uweza wa Mungu kama huo, anao ushindi taayari upande wake.  Kwa maana, tazama, Yehoshafati sio tu alikiri limani yake katika uweza wa ajabu wa Mungu, bali aliidai nguvu ya Mungu kama ni yake mwenyewe, akisema,  "Si wewe,  Ee  MUNGU WETU?"  Alitimiza matakwa ya Maandiko:  "Kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba Yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao."

     Kisha Yehoshafati akaendelea kusimulia jinsi BWANA alivyowakalisha katika nchi ile,  na kwamba, ijapokuwa hakuwaruhusu kuwashambulia Wamoabu na Waamoni, mataifa hayo yalikuwa yamekuja kuwatupa toka milki yake aliyowarithisha.   Fungu la 7-ll.  Kisha ndipo alipomaliza kwa kusema:  "Ee Mungu wetu, je!  hutawahukumu?  maana sisi hatuna uwezo juu ya jamii kubwa  hii, wanaotujia juu yetu;  wala hatujui tufanyeje;  lakini macho yetu yatazama kwako."  Fungu la l2.  Si kitu kwa  BWANA kusaidia, akiwa  pamoja na wengi, ama akiwa pamoja na wale wasiokuwa na uwezo (2 Nya. l4:ll);  kwa maana macho ya BWANA hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe Mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea Kwake (2 Nya.l6:9), basi, ni vyema  kwa wale walio katika shida kumtegemea Yeye  peke yake.  Msimamo wa Yehoshafati na watu wake ulilingana na agizo lile la mtume,  "Tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu."  Ebr.l2:2.  Yeye ndiye Mwanzo na Mwisho, na mamlaka yote mbinguni na duniani amepewa Yeye.

     Sasa, je!  matokeo yalikuwaje?  ----  Nabii wa Mungu alikuja katika nguvu ya Roho Mtakatifu, "akasema,  Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati;  BWANA  awaambia hivi,  Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili;  kwani vita si yenu bali ni ya Mungu."  Fungu la l5.  Kisha amri ikatolewa ya kuwashukia  adui zao asubuhi iliyofuata, na ya kwamba watauona wokovu wa BWANA, kwa maana atakuwa pamoja nao.

     Sasa inakuja sehemu ya muhimu sana:-

     "Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda  katika jangwa la Tekoa;  nao walipokuwa wakitoka,  Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu;  mwaminini BWANA

Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika;  waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.  Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia  BWANA, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema  Mshukuruni  BWANA;  kwa maana fadhili zake ni za milele."  Fungu la 20, 2l.

     Kwa hakika hii ilikuwa mbinu ya ajabu kwenda vitani.  Ni majeshi machache mno yanayokwenda vitani yakiwa na kikosi cha mstari wa mbele kama hicho.  Lakini, je!  matokeo yalikuwaje?

     "Nao walipoanza kuimba na kusifu,  BWANA akaweka waviziao  juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda;  nao wakapigwa.  Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima  Seiri  kuwaulia mbali na kuwaharibu;  nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe.  Hata Yuda walipofika mnara wa kulindia wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi;  nao, angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka."  Fungu la 22-24.

     Iwapo majeshi machache mno yamepata kuwako ambayo yameenda vitani na kikosi cha mstari wa mbele kama hicho  kama  lilivyofanya jeshi la Yehoshafati, basi, vivyo hivyo ni hakika kuwa ni majeshi machache mno yaliyopewa ushindi mkuu kama huo.  Na huenda isiwe vibaya kutafiti zaidi kidogo falsafa hii ya ushindi wa imani, kama kielelezo kilivyotolewa katika mfano huu.  Adui, ambao walikuwa na imani nyingi juu ya ubora wa jeshi lao kubwa, walipowasikia Waisraeli wakija asubuhi ile,  huku wakiimba na kupiga  makelele, unafikiri walifikia uamuzi  gani?  ----  Hawakuwa na uamuzi mwingine wo wote ila ule  wa kwamba  Waisraeli walikuwa wamepata askari wengine  wa kuongeza nguvu ya jeshi lao, na kwamba walikuwa wametiwa nguvu sana hata ilikuwa ni bure kabisa kujaribu kuwapinga.  Basi, hofu kuu ikawashika, na kila mmoja akamwona jirani yake kama adui yake.

     Je,  hawakuwa sawa katika uamuzi wao, kwamba Israeli ilikuwa imepokea askari wengi zaidi wa kuwaongezea nguvu?  ----  Naam, walikuwa wamepokea;  maana habari inasema:  "Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA AKAWEKA WAVIZIAO juu ya wana wa Amoni,  na Moabu, na wa mlima Seiri."  Jeshi la BWANA, ambalo Yehoshafati na watu wake walilitumainia, likawapigania.  Walipata askari zaidi wa kuwaongezea nguvu, na bila shaka kama macho yao yangeweza kufumbuliwa ili kuwaona, wangeweza kuona kama alivyoona yule mtumishi wa Elisha wakati wa tukio moja, kwamba wale waliokuwa pamoja nao walikuwa wengi zaidi kuliko  idadi ya adui zao.

     Lakini jambo moja ambalo halina budi kuangaliwa kwa makini ni kwamba ilikuwa wakati ule Israeli walipoanza kuimba na kusifu, ndipo Bwana  akaweka waviziao juu ya adui.  Hii inaashiria nini?   ----  Inaashiria kwamba imani yao ilikuwa ya kweli.  Ahadi ya Mungu ilihesabiwa kuwa ni sawasawa na ushindi halisi.  Basi, wakamwamini Bwana, ama kwa maana iliyo wazi, walijenga juu ya Bwana, na hivyo waliimarishwa, ama, walijengwa.  Kwa njia  hiyo waliithibitisha kweli ya maneno haya,  "Na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu."  l Yohana 5:4.

     Hebu sasa na tukitumie kielelezo  hiki katika jambo la  kupambana na dhambi.  Hapa jaribu lenye nguvu linakuja kwetu ili tufanye tendo lijulikanalo kuwa ni dhambi.  Mara nyingi tumeshuhudia kwa masikitiko nguvu ya jaribu hilo, kwa sababu limetushinda, hata tunajua kwamba sisi hatuna nguvu ya kulipinga.  Lakini sasa hivi macho yetu yako juu ya  Bwana, ambaye ametuambia tukikaribie kiti chake cha rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.  Basi, tunaanza kumwomba Mungu yule aliyefunuliwa kwetu katika Biblia kama Muumbaji wa mbingu na nchi.  Tunaanza, sio kwa maneno ya kuomboleza kwa ajili ya udhaifu wetu, bali kwa kukiri kwa furaha uweza mkuu wa Mungu.  Hilo likiwa limekwisha, hapo ndipo tunapoweza kuthubutu kueleza shida yetu  na  udhaifu wetu.  Tukieleza udhaifu wetu kwanza, na hali ya kukatisha tamaa inayotuzunguka, basi, tunakuwa tumejiweka wenyewe mahali pa Mungu.  Katika hali kama  hiyo Shetani ataikuza sana shida yetu na kututupia giza lake kutuzunguka ili tusiweze kuona kitu kingine cho chote isipokuwa udhaifu wetu peke yake, na kwa hiyo, ingawa kilio chetu na kusihi kwetu vinaweza kutolewa kwa nguvu zote na kuugua, itakuwa ni bure kabisa, kwa sababu kitapungua kitu kile cha muhimu cha kuamini kwamba Mungu yuko, na kwamba yuko kama vile alivyojidhihirisha mwenyewe.  Lakini hapo tunapoanza kwa kuutambua uweza wa Mungu,  ndipo kwa usalama tuwezapo kueleza udhaifu wetu, maana kwa wakati huo tunachofanya tu ni kule kuuweka udhaifu wetu sambamba na uweza Wake, katika kupambanisha  unazaliwa ujasiri ndani yetu.

     Halafu, wakati sisi tunapoomba, huja moyoni mwetu ahadi ya Mungu,  inaletwa humo na Roho Mtakatifu.  Huenda tusiwe na mawazo yo yote juu ya ahadi maalum ambayo inafaa kabisa kwa shida yetu;  lakini tunaweza kukumbuka ya kwamba  "Ni nelo la  kuaminiwa, na tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi" (l Tim.l:l5);  na ya kwamba "alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu."  (Gal.l:4);  nasi tunaweza kujua jambo hilo kwambaa ndani yake lilikuwa na kila ahadi, kwa maana,  "Yeye asiyemwachilia Mwana Wake Mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?"  Rum.8:32

     Kisha tunakumbuka kwamba Mungu anaweza kusema juu ya mambo yale ambayo hayapo kana kwamba yapo.  Yaani, Mungu  atoapo ahadi, ni sawa na kutimizwa tayari kwa ahadi hiyo.  Hivyo, basi, tukijua kwamba ukombozi wetu kutoka dhambini ni kwa mapenzi ya Mungu (Gal.l:4), tunauhesabu ushindi kama ni wetu tayari, nasi papo hapo tunaanza kumshukuru Mungu kwa ajili ya "ahadi [zake] kubwa mno, za thamani."  Imani yetu izishikapo ahadi hizi na kuzihesabu kuwa ni za kweli, ndipo hatuwezi kujizuia kumshukuru Mungu kwa upendo wake wa ajabu;  na tunapofanya hivi, hapo ndipo mawazo yetu yanaondolewa mbali kabisa na maovu, na ushindi unakuwa wetu.  Bwana huweka waviziao  juu ya adui.  Kule kutoa sifa kwetu humdhihirishia Shetani kwamba sisi tumepata nguvu mpya nyingine ya kutupatia ushindi;  na kwa vile amekwisha kuionja nguvu hiyo ya msaada unaotolewa kwetu, anajua kwamba hawezi kufanya lo lote kwa  tukio kama hilo, na kwa hiyo anatuacha.  Hiki ndicho kielelezo cha nguvu ya agizo la mtume:-

     "Msijisumbue kwa neno lo lote, bali katika kila neno kwa kusali na kuomba PAMOJA NA KUSHUKURU,  haja zenu na zijulikane na Mungu."  Wafilipi  4:6.