>Mwanzo >Soma vitabu >Kristo na haki yake >Kristo kama muumbaji

Kristo kama muumbaji

KRISTO KAMA MUUMBAJI

 

     Mara tu baada ya fungu linalodondolewa mara kwa mara lisemalo kwamba Kristo, Neno, ni Mungu, tunasoma kwamba "Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo Yeye hakukufanyika cho chote kilichofanyika."  Yohana 1:3.  Maelezo yo yote hayawezi kuufanya usemi huo kuwa wazi zaidi kuliko ulivyo, kwa hiyo, tunasonga mbele kwenda kwenye maneno ya Waebrania 1:1-4: "Mungu ... mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa Yeye aliufanya ulimwengu.  Yeye kwa kuwa ni mng' ao wa utukufu wake, akiisha kuufanya utakaso wa dhambi, alikaa mkono wa kuume wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilorithi lilivyo tukufu kuliko lao."

     Tena mkazo zaidi kuliko huu umetolewa katika maneno ya Paulo kwa Wakolosai.  Akizungumza juu ya Kristo kama Mmoja ambaye kwa njia yake tunao ukombozi, anamweleza kama Mmoja ambaye ni "mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.  Kwa kuwa katika Yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka;  vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake.  Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika Yeye." Kol.1:15-17.

     Fungu hili la ajabu halina budi kujifunzwa kwa uangalifu na kutafakariwa mara kwa mara.  Haliachi kitu hata kimoja katika ulimwengu ambacho Kristo hakukiumba.  Aliumba kila kitu kinachoweza kuonekana, na kila kitu kisichoweza kuonekana; viti vya enzi, usultani, enzi, na mamlaka mbinguni, vyote hivi humtegemea Yeye kwa kuwako kwavyo.  Na kwa kuwa amekuwako kabla ya vitu vyote, na Yeye ndiye Muumbaji wa hivyo, basi, katika Yeye vitu vyote hushikana ama hushikamana pamoja.  Usemi huu ni sawa na ule uliosemwa katika Ebr.1:3, kwamba anavichukua vyote kwa amri ya uweza wake.  Ni kwa njia ya Neno mbingu ziliumbwa;  na ni Neno yule yule anayezishikilia mahali pake, na kuzilinda zisiharibike.

     Tukiwa katika wazo hili hatuwezi kuacha Isa.40:25,26:  "Mtanifananisha na nani, basi, nipate kuwa sawa naye? asema Yeye aliye Mtakatifu.  Inueni macho yenu juu, mkaone;  ni nani aliyeziumba hizi;  aletaye nje jeshi lao kwa hesabu;  aziita zote kwa majina;  kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa Yeye ni hodari kwa nguvu zake;   hapana moja isiyokuwapo mahali pake."  Ama, kama tafsiri ya Kiyahudi inavyoeleza kwa nguvu zaidi,  "Kwake, aliye na uweza mkuu, na mwenye nguvu, hapana moja isiyokuwapo mahali pake."  "Kwamba Kristo ni Yule Mtakatifu aliitaye jeshi lote la mbinguni kwa majina, na kulishikilia mahali pake, ni dhahiri kutokana na sehemu nyingine za sura hiyo.  Yeye Ndiye ambaye mbele zake ilisemwa, "Itengenezeni nyikani njia ya Bwana; Nyosheni jangwani njia kuu  kwa Mungu wetu."  Yeye Ndiye ajaye aliye na mkono wa nguvu, aliye na ujira wake pamoja naye;  Ndiye, aliye kama mchungaji, alilishaye kundi lake,  akiwachukua wana kondoo kifuani pake.

     Usemi mmoja zaidi unaomhusu Kristo kama Muumbaji utatutosha.  Ni ushuhuda wa Baba Mwenyewe.  Katika sura ya kwanza ya Waebrania, tunasoma kwamba Mungu amesema na sisi katika Mwana; alisema kwa habari zake,  "Afanyaye malaika zake kuwa pepo, na watumishi wake kuwa miali ya moto," lakini kwa habari za Mwana asema,  "Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele;  Na fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili;" na Mungu asema tena:  "Wewe, Bwana, hapo mwanzo uliitia misingi ya nchi; Na mbingu ni kazi za mikono yako."  Ebr.1:8-10.  Hapa tunamwona Baba akimwambia Mwana kuwa ni Mungu, na kumwambia, Wewe uliitia misingi ya nchi; na mbingu ni kazi za mikono yako.  Mungu Baba Mwenyewe anapompa heshima hii Mwanawe, mwanadamu ni kitu gani hata azuie kumpa heshima hii?  Kwa wazo hili tunaweza kuuacha ushuhuda wa moja kwa moja kuhusu Uungu wake Kristo, na ukweli kwamba Yeye ndiye Muumbaji wa vitu vyote.

     Neno la tahadhari huenda likawa la muhimu kulisema  hapa.  Hebu asiwepo mtu ye yote anayefikiri kwamba tungeweza kumtukuza Kristo kwa hasara ya Baba, ama kwa kutomjali Baba.  Hilo haliwezakani, kwa maana mambo yao ni mamoja.  Tunamheshimu Baba kwa kumheshimu Mwana.  Tunayakumbuka maneno ya Paulo aliposema "kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake, nasi tunaishi kwake;  yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo, na sisi kwa Yeye huyo."  (1 Kor.8:6); kama tulivyodondoa tayari, ni kwa Yeye Mungu aliumba ulimwengu.  Vitu vyote hatimaye hutoka kwake Mungu, Baba;  hata Kristo Mwenyewe alitoka na kuja kutoka kwa Baba;  lakini imempendeza Baba kwamba katika Yeye (Kristo) unakaa utimilifu wote wa Mungu, na kwamba Yeye awe ndiye Mtendaji wa karibu anayesimamia kila tendo la uumbaji.  Kusudi letu katika uchunguzi huu ni kumweka Kristo katika cheo chake halali cha kuwa sawa na Baba, ili uweza wake wa kukomboa uweze kuthaminiwa vizuri zaidi.