>Mwanzo >Masomo >Nifanye nini ili niokoke?

Nifanye nini ili niokoke?

Yanipasa  Nifanye  Nini Nipate Kuokoka?

 

E. G. WHITE
 

     “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!” (Yohana 1:29).  Narudia kuyasema maneno ya Yohana,  “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu!”   Tunatakiwa kuiangalia sana tabia yake Kristo.  Tunapaswa kutafakari juu ya msalaba ule wa Kalvari;  maana huo ndio hoja ya Ukristo isiyokanushika.  Ujumbe wa Mungu ni huu kwa mwenye toba, na onyo lake kwa yule anayerudi nyuma ni hili,  “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!”  Wale wanaompelekea mtu ujumbe huo huenda wakaweza kugeukia kando na kuiacha kweli hiyo, lakini yule anayetaka kuokolewa hana budi kukaza jicho lake kwa Yesu.  Kwa kumtazama Kristo atajifunza kuichukia dhambi yake, ambayo imemletea mateso na mauti Mkombozi wake.  Kwa kutazama, imani yake hupata nguvu, naye anakuja kumjua “Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo [a]liyemtuma” (Yohana 17:3).  Mwenye dhambi humwona Yesu kama vile alivyo hasa, yaani, mwingi wa huruma na upendo, na kwa kuuona upendo huo mkuu wa Mungu katika mateso ya Kristo pale msalabani ambao umedhihirishwa kwa mwanadamu aliyeanguka [dhambini] anabadilika tabia yake.

     Wakati ambapo wokovu wetu hutegemea kabisa juu ya Yesu, bado sisi tunayo kazi ya kufanya ili tupate kuokoka.  Mtume anasema,  “Utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.  Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema” (Wafilipi 2:12,13).  Kazi tunayotakiwa kufanya si kazi ya kujitegemea wenyewe mbali na kazi ile anayotaka kufanya Mungu [ndani yetu], bali ni kazi ya kushirikiana na Mungu.  Uweza na Neema ya Mungu hutumiwa na Mtendakazi huyo wa Mbinguni ndani ya moyo;  lakini hapa ndipo wengine hupotea, wakidai kwamba mwanadamu anayo kazi ya kufanya ambayo ni ya kujitegemea mwenyewe kabisa bila kushirikiana na kazi yo yote anayotenda Mungu [ndani yake].  Kundi lingine huvuka mpaka na kwenda upande mwingine, na kusema kwamba mwanadamu hawajibiki kabisa, ati kwa sababu Mungu anafanya kazi yote  -  kutaka na kutenda.  Lakini sababu ya kweli tunayotakiwa kuifuata ni ile isemayo kwamba nia [mapenzi] ya mwanadamu inapaswa kuitii nia [mapenzi] ya Mungu.  Nia ya mwanadamu haipaswi kulazimishwa ili ipate kushirikiana na  wajumbe wale aliowaweka Mungu, bali inapaswa kunyenyekea kwa hiari.  Mwanadamu hana uwezo wo wote ndani yake wa kumwezesha kuutimiza wokovu wake mwenyewe.  Wokovu ni lazima uwe ni matokeo ya kushirikiana na uweza wa Mungu;  na Mungu hawezi kumfanyia mwanadamu kile mwanadamu anachoweza kujifanyia mwenyewe.  Mwanadamu anategemea kabisa neema ya Kristo.  Hana nguvu ya kusogea hatua moja kuelekea kwa Kristo isipokuwa kama Roho wa Mungu anamvuta kwake [Kristo].  Lakini Roho Mtakatifu wakati wote anamvuta mwanadamu huyo, tena ataendelea kumvuta mpaka hapo mwenye dhambi huyo atakapoendelea kukataa kuvutwa na kumhuzunisha na kumfukuza Mjumbe huyo Mpole wa Mungu.

     Katika mabaraza yale ya mbinguni maamuzi yamekwisha kufanywa juu ya njia na mbinu zitakazotumika ili neema ya Kristo iweze kuleta matokeo yanayofaa katika kumwokoa mwanadamu.  Tena ni wazi kwamba mwenye dhambi huyo asipokubali kuvutwa, yaani, asiposhirikiana na njia alizoziweka Mungu, basi, lengo lililokusudiwa halitaweza kufikiwa. Kazi inayotakiwa kufanywa ni kazi ya kushirikiana pamoja.  Mungu na mwanadamu wanapaswa kufanya kazi pamoja, na mwenye dhambi hana budi kutegemea Neema wakati anaendelea kutoa utii wake kwa hiari kulingana na maongozi ya Roho wa Mungu.  “Utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.  Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.”

     Mungu amewapa wanadamu akili na uwezo wa kuzitumia akili zao, lakini kama akili haifanyiwi mazoezi, yaani, inaachwa bila kuielimisha, basi, wanadamu watakuwa kama washenzi wasiostaarabika.  Akili ni lazima ipatiwe elimu, ni muhimu kwamba waalimu wafundishe mstari kwa mstari, kanuni juu ya kanuni, wakimwongoza na kumfunza mjumbe huyo mwenye maadili ili apate kuelewa maana ya kushirikiana na Mungu.  Mungu anafanya kazi ndani ya mjumbe wake wa kibinadamu kwa njia ya nuru ya ile kweli [Yoh. 17:17], na akili yake ikielimishwa kwa ile kweli inakuwa na uwezo wa kuiona kweli kwa kuibainisha na uongo.  Moyo ukiachwa wazi kuipokea nuru ya ile kweli, ukiwa hauna chuki isiyo na sababu dhidi ya kweli hiyo, ukiwa haufungwi na mawazo na desturi za wanadamu, basi, moyo huo ulioelimishwa hivyo utauona waziwazi ushahidi wa ile kweli, na kuiamini kama inatoka kwa Mungu.  Mtu aliyeelimishwa na ile kweli hataweza kuuita uongo kuwa ndiyo kweli, wala nuru kuwa ndilo giza.   Roho anaufunulia moyo wake mambo ya Mungu, na kwa yule anayeshirikiana na Mungu, atatambua kwamba kuwako kwake Mungu kunamzunguka juu yake.  Moyo wake unapofunguliwa kumpokea Yesu na akili yake inapoikubali ile kweli, Yesu hukaa moyoni mwake.  Nguvu ya Roho hufanya kazi ndani ya moyo wake, na kuifanya mielekeo ya moyo wake ipate kumwelekea Yesu.  Kwa imani ile iliyo hai, Mkristo huyo huutegemea kabisa uwezo wa Mungu, akitazamia kwamba Mungu atamwezesha “kutaka” na “kutenda” kile kitakacholitimiza kusudi lake jema.  Mara tu mtu anapoamua la kufanya na kulitenda kulingana na nuru iliyofunuliwa kwake, Roho huyatwaa mambo ya Mungu na kumpa mtu huyo nuru nyingi zaidi. 

     “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.”  “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu;  nasi tukauona utukufu wake [tabia yake takatifu – Kut. 33:18,19;  34:5-7;  1 Yoh. 4:8], utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba;  amejaa Neema na Kweli.”  Yohana 1:12,14.  Roho wa Mungu hajatumwa kufanya sehemu ya kazi inayotuhusu sisi, yaani, kutaka kwetu, ama kutenda kwetu [yaani, ni lazima sisi wenyewe tutake na kutenda; tukifanya hivyo, yeye anatupa uwezo wa kufanya mambo hayo mawili].  Ni kazi ya mjumbe wa kibinadamu kushirikiana na wajumbe wale wa mbinguni.  Mara tu tunapoyaelekeza mapenzi yetu ili yaweze kupatana na yale ya Mungu, neema ya Kristo hutolewa kwetu kushirikiana nasi katika maamuzi yetu tuliyofanya.  Lakini neema hiyo haikusudiwi kuwa badala ya kazi yetu  -  yaani, haiwezi kufanya kinyume na maamuzi yetu [tuliyofanya] na matendo yetu [tunayofanya].  Kwa  hiyo, mafanikio yetu katika maisha yetu ya Kikristo hayatapatikana kwa sababu ya wingi wa nuru na ushahidi tuliopewa, bali utategemea juu ya kuikubali kwetu nuru hiyo tuliyopewa, itategemea jinsi tutakavyoziamsha nguvu zetu, na kufanya kazi yetu pamoja na wahudumu wa mbinguni [malaika] waliochaguliwa na Mungu kufanya kazi kwa ajili ya wokovu wetu [Ebr. 1:14].

     Kama mwenye dhambi au yule aliyerudi nyuma anaendelea kujituliza katika dhambi, basi, nuru ile ya mbinguni inaweza kuwa inamulika kumzunguka pande zote, lakini bila faida yo yote kwake, kama ilivyofanya kwa Sauli [Paulo] wakati udanganyifu wa ulimwengu huu unaopumbaza akili [unaoduwaza] ulipomkalia.  Mjumbe wa kibinadamu asipoyaelekeza mapenzi yake kufanya mapenzi ya Mungu, kama alivyofanya Sauli [Paulo] hatimaye, basi, nuru hiyo itang’aa bila faida yo yote kwake, na hata kama atapata nuru na ushahidi mara elfu zaidi, mambo hayo hayatamletea jema lo lote.  Mungu anajua ni wakati gani mwenye dhambi anapokuwa amepata ushahidi wa kutosha, na kwa watu hao anawaambia hivi:  “Wanao Musa na manabii;  na wawasikilize wao [yaani, wanayo Biblia na waisikilize na kuitii]. “Wasipowasikiliza Musa na manabii [wasipoisikiliza na kuitii Biblia], hawatashawishiwa hata mtu akifufuka katika wafu” (Luka 16:29,31).

     Paulo alizinduka kwa hofu kuu baada ya kummulikia nuru ile iliyotoka mbinguni, na sauti ilipomwambia,  “Sauli, Sauli, mbona waniudhi [wanitesa]?  Paulo akajibu, akasema,  “U nani wewe, Bwana?”  Naye akasema,  “Mimi ndimi Yesu unayeniudhi [unayenitesa – Zek. 2:8];  ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo” [Mdo. 26:14].  Kisha Bwana akamwambia,  “Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda” (Matendo 9:4-6].  Daima Bwana humpa mjumbe wake wa kibinadamu kazi ya kufanya.  Paulo alitakiwa kufanya kazi yake kwa kuitii amri ya Mungu.  Lakini basi, hebu na tuseme yeye angesema hivi:  “Bwana, sijisikii kabisa kuyafuata maagizo yako katika kuutimiza wokovu wangu,”  halafu, Bwana angemmwagia nuru juu yake inayong’aa mara kumi zaidi, nuru hiyo ingekuwa kazi bure kwake.  Ni jukumu la mwanadamu kushirikiana na Mungu.  Hapo ndipo ambapo pambano linapotakiwa kuwa kali sana, gumu sana, na la kikatili sana  -  katika kuchukua jukumu letu la kuyasalimisha mapenzi na njia yetu chini ya mapenzi na njia ya Mungu, kwa kutegemea mivuto ya neema yake ambayo Mungu anaitumia katika moyo wa mwanadamu katika maisha yake yote.  Mwanadamu ni lazima afanye kazi yake ya KUTAKA.  “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu,  kutaka kwenu [ni lazima kwanza sisi tutake] na kutenda kwenu [ni lazima tuanze kutenda kile tunachotaka kufanya kabla uweza wake haujaanza kufanya kazi yake kushirikiana nasi].”  Aina ya matendo tunayotenda itathibitisha aina ya maamuzi tuliyofanya.  Tutaona kwamba utendaji wetu haukuwa sawa na hisia zetu [tunavyojisikia moyoni], wala na mwelekeo wetu wa kawaida, bali ulipatana na mapenzi ya Baba yetu aliye mbinguni.  Fuateni na kuyatii maongozi ya Roho Mtakatifu;  msiitii sauti ya yule laghai [Shetani] inayolandana na mapenzi yetu yasiyotakaswa [yaani, ya dhambi], bali utiini ule msukumo wa kutaka aliouweka Mungu ndani yenu.  Hiyo ndiyo kazi wanayoifanya daima wenye hekima wale wa mbinguni [malaika] katika kutusaidia sisi kutenda  -  yaani, kufanya mapenzi ya Baba yetu aliye mbinguni.

     Vita dhidi ya nafsi [kujipenda wenyewe/uchoyo], hilo ndilo pambano kuu kuliko yote lililopata kupiganwa.  Kuisalimisha nafsi [kukubali umimi ufe kabisa], yaani, kuacha vyote kwa madhumuni ya kutimiza mapenzi ya Mungu, huhitaji jitihada ifanyike, lakini ni lazima moyo ujisalimishe kwanza kwa Mungu kabla ya kuweza kufanywa upya katika hali ya utakatifu.

     Mungu halazimishi mapenzi ya viumbe vyake ili yamwelekee yeye.  Hawezi kukubali utii [wa mtu ye yote] ambao haujatolewa kwa hiari yake na kuamuliwa kwa akili yake mwenyewe.   Kutii kwa kujilazimisha tu kungeweza kuzuia maendeleo yote ya akili na tabia.  Kungeweza kumfanya mwanadamu kuwa kama roboti [mashine kama mwanadamu inayojiendesha yenyewe].  Hilo si kusudi la Muumbaji wetu alilo nalo kwetu sisi.  Anayo shauku kubwa kwamba mwanadamu aliye kilele cha uweza wake wa uumbaji, apate kufikia ukuaji [wa tabia yake] wa kiwango cha juu kabisa iwezekanavyo.  Anaweka mbele yetu kimo cha mbaraka ule anaotamani kutupatia ili kutuwezesha kukifikia kwa njia ya neema yake.  Anapenda sisi tujisalimishe wenyewe [yaani, kwa hiari yetu] kwake, ili apate kutenda mapenzi yake ndani yetu.  Ni juu yetu [kazi kwetu] kuchagua kuwekwa huru mbali na dhambi, na kuingia katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.

     Mnachohitaji kuelewa ni uwezo [nguvu] halisi wa nia yenu.  Hiyo ndiyo nguvu inayotawala tabia ya mwanadamu,  hiyo ndiyo uwezo wa kukata shauri [kuamua unalotaka kufanya], au uwezo wa kuchagua [la kufanya].  Kila kitu hutegemea juu ya utendaji sahihi wa NIA ya mtu.  Uwezo huo wa kuchagua wanadamu wamepewa na Mungu;  ni wao wanaopaswa kuutumia.  Wewe huwezi [huna uwezo wa] kuugeuza moyo wako, huwezi [huna uwezo] wewe mwenyewe kuyasalimisha kwa Mungu mapenzi yako yaliyomo moyoni mwako;  lakini unaweza kuchagua [kuamua moyoni mwako kuwa unataka] kumtumikia yeye.  Ninyi mnaweza kumpa nia [mapenzi] yenu;  hapo ndipo yeye atakapotenda kazi yake ndani yenu, [na kuwawezesha ninyi kutimiza] kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema [la kuwaokoa ninyi].  Kwa njia hiyo, tabia yenu yote itawekwa chini ya udhibiti [utawala] wa Roho wake Kristo;  mapenzi yenu yataelekezwa yote kwake;  mawazo yenu yote yatapatana na yake.

     Kwa kuitumia vizuri nia yako [yaani, kutaka kwako], badiliko kamili linaweza kutokea katika maisha yako.  Kwa kusalimisha mapenzi [nia] yako kwa Kristo, unajiunganisha na nguvu ile ipitayo falme na mamlaka zote [yaani, Kristo].  Utakuwa na nguvu itokayo juu ya kukushikilia imara, na hivyo kwa kuendelea daima kusalimisha nia [mapenzi] yako kwa Mungu utawezeshwa kuishi maisha mapya, yaani, maisha yale ya imani.

     Kila kitu kiko hatarini.  Je!  mjumbe [wakala] huyo wa kibinadamu atapenda kushirikiana na wajumbe wale wa Mungu [malaika] ili apate kutaka na kutenda [ipasavyo]?  Kama mwanadamu huyo ataweka nia [mapenzi] yake upande ule unaolandana na nia [mapenzi] ya Mungu, yaani, akiisalimisha nafsi yake kabisa ili apate kufanya mapenzi yake [Mungu], hapo ndipo takataka zitakapondolewa kutoka mlangoni pa moyo wake, ukaidi wa moyo wake utavunjiliwa mbali, na Yesu ataingia humo kukaa kama Mgeni [rasmi] aliyekaribishwa.

 

     Mrs. E. G. White,  What Must I Do to Be Saved?, originally “Apples of Gold No. 17, October 1894

     Kiswahili – Yanipasa Nifanye Nini Nipate Kuokoka?  Tr. M. Mwamalumbili.

Related Information