>Mwanzo >Masomo >Kubadirishwa kwa Neema

Kubadirishwa kwa Neema

KUBADILISHWA KWA NEEMA

 

ELLEN  G.  WHITE

 

     Katika maisha ya mwanafunzi Yohana utakaso wa kweli unaonyeshwa kama kielelezo.  Katika miaka ile alipokuwa na uhusiano wa karibu sana na Kristo, mara nyingi alionywa na kushauriwa na Mwokozi;  na makaripio yale aliyapokea. Tabia yake Yule wa Mbinguni [Kristo] ilipodhihirishwa kwake, Yohana aliutambua upungufu aliokuwa nao, ufunuo huo ukamfanya apate kunyenyekea.  Siku kwa siku, akiwa anailinganisha na tabia yake ya ukali, aliweza kuona huruma na uvumilivu wa Yesu, na kuyasikia mafundisho yake juu ya unyenyekevu na uvumilivu.  Siku kwa siku moyo wake ulivutwa kwa Kristo, hadi alipoifikia hali ya kuisahau nafsi yake kutokana na upendo aliokuwa nao kwa Mwokozi wake. Aliona katika maisha ya kila siku ya Mwana wa Mungu uweza na huruma, ukuu na upole, nguvu na uvumilivu, moyo wake ukajazwa na mshangao.  Alikiri kwamba tabia yake ya hasira na kutaka makuu ilikuwa haina budi kubadilishwa kwa uweza wake Kristo, ndipo upendo wa Mungu ulipotenda kazi ndani yake na kumletea badiliko katika tabia yake.

     Kinyume cha kushangaza sana cha utakaso ule uliofanyika katika maisha ya Yohana ni uzoefu wa maisha ya mfuasi yule mwenzake, yaani, Yuda. Yuda, kama yule mwenzake, alijiita mfuasi wa Kristo, lakini alikuwa na mfano tu wa utauwa.  Si kwamba hakuujua uzuri wa tabia yake Kristo; mara nyingi, aliposikiliza maneno ya Mwokozi, aliona hatia, lakini hakutaka kujinyenyekeza moyoni mwake, wala kuziungama dhambi zake.  Kwa kuupinga mvuto ule wa Mungu alimwaibisha Bwana wake ambaye yeye alikiri kuwa anampenda. Yohana kwa bidii akapigana na makosa yake;  lakini Yuda akatenda kinyume na dhamiri yake na kuanguka majaribuni, akiyafunga ndani yake kwa uthabiti zaidi mazoea yake ya dhambi.  Kuziweka katika maisha [matendo] yake kweli zile alizofundisha Kristo kukawa hakupatani kabisa na tamaa zake na makusudi yake, naye hakuweza kujilazimisha kuachana na mawazo yake ili kupokea hekima ile itokayo mbinguni.  Badala ya kwenda nuruni, akachagua kwenda gizani.  Tamaa yake mbaya, uchoyo wake [kujipenda nafsi], shauku yake ya kulipiza kisasi, mawazo yake ya giza na ukaidi wake, yote hayo akayalea [akayatunza] moyoni mwake mpaka Shetani akapata nafasi ya kumtawala kabisa.

     Yohana na Yuda ni wawakilishi wa wale wanaojiita wafuasi wa Kristo.  Wanafunzi hawa wawili walikuwa na nafasi zile zile za kuweza kujifunza kumfuata yule aliye Kielelezo cha utakatifu.  Wote walishirikiana kwa karibu sana na Yesu, tena walikuwa na bahati ya kuyasikia mafundisho yake.  Kila mmoja alikuwa na kasoro kubwa katika tabia yake;  na kila mmoja alikuwa na haki ya kuipokea neema ya Mungu inayobadili tabia.

  Lakini wakaati yule mmoja kwa unyenyekevu wa moyo alikuwa akijifunza kumjua Yesu, yule mwingine alijionyesha waziwazi kuwa alikuwa si mtendaji wa neno, bali msikiaji tu.  Mmoja, akiwa anakufa [anaifisha nafsi yake] kila siku na kuishinda dhambi, alitakaswa kwa njia ya ile kweli;  yule mwingine, akiupinga uweza wa neema unaobadili tabia na kujiachilia kutimiza tamaa zake za uchoyo, alijikuta amekuwa mtumwa wa Shetani. 

     Badiliko katika tabia kama lile lililoonekana katika maisha ya Yohana daima huwa ni matokeo ya kushirikiana na Kristo.  Huenda kasoro zinazoonekana wazi katika tabia ya mtu zikaweza kuwapo, licha ya hizo, anapokuwa mfuasi wa kweli wa Kristo, uwezo wa neema ya Mungu huibadili tabia yake na kumtakasa.  Anapouangalia utukufu wa Bwana kama katika kioo, anabadilishwa [tabia yake] toka utukufu hata utukufu, mpaka anafanana kabisa na yeye anayemwabudu [2 Kor. 3:18].

     Yohana alikuwa ni mwalimu aliyefundisha utakatifu, na katika nyaraka zake kwa kanisa aliweka kanuni zisizokosea za mwenendo unaofaa kwa Wakristo.  “Na kila mwenye matumaini haya,” aliandika, “katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu.”  “Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda.”  1 Yohana 3:3;  2:6.  Alifundisha kwamba Mkristo ni lazima awe safi katika moyo wake na katika maisha yake.  Kamwe asiridhike na imani tupu [yaani, isiyokuwa na matendo].  Kama vile Mungu alivyo Mtakatifu katika mazingira yake, ndivyo, mwanadamu yule aliyeanguka [dhambini], anavyopaswa kuwa mtakatifu katika mazingira yake.

     “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu,” aliandika Mtume Paulo, “kutakaswa kwenu.”  1 Wathesalonike 4:3.  Utakaso wa kanisa lake ndilo lengo alilo nalo Mungu katika kushughulika kwake kote na watu wake.  Amewachagua tangu milele, ili wapate kuwa watakatifu.  Alimtoa Mwanawe kuwafia, ili wapate kutakaswa kwa njia ya kuitii ile kweli, wakiwa wamevuliwa unyonge wote wa nafsi zao.  Kutoka kwao anataka kazi ya [yaani, utendaji wa] kila mtu peke yake;  yaani, kila mtu kujisalimisha mwenyewe kwake.  Mungu anaweza kupewa utukufu na wale wanaodai kuwa wanamwamini wakati ule tu wanapofanana na sura [tabia] yake na kutawaliwa na Roho wake.  Hapo ndipo, wao wakiwa ni mashahidi wake Mwokozi, wanaweza kutangaza kwa wengine kile ilichowafanyia neema ya Mungu.

     Utakaso  wa  kweli  unakuja kwa njia ya utendaji wa kanuni ile ya upendo.  “Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, Mungu hukaa ndani yake.”  

1 Yohana 4:16.  Maisha ya mtu yule ambaye moyoni mwake Kristo anakaa, yataonyesha utauwa kwa matendo.  Tabia yake itatakaswa, itakuwa bora, itaadilishwa, na kutukuzwa.  Mafundisho safi ya dini yatapatana na matendo ya haki;  kanuni za mbinguni zitachanganyika pamoja na matendo matakatifu ya maisha.

     Wale ambao wangetaka kupata mbaraka huo wa utakaso inawapasa kwanza kujifunza maana ya kujinyima.  Msalaba wa Kristo ni nguzo ya katikati ambayo juu yake unaangikwa “utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana.”  “Mtu ye yote akitaka kunifuata,”  Yesu asema,  “ na ajikane  mwenyewe,  ajitwike  msalaba  wake,  anifuate.”  

2 Wakorintho 4:17;  Mathayo 16:24.  Ni ile harufu nzuri ya upendo wetu kwa wanadamu wenzetu inayoudhihirisha upendo wetu kwa Mungu.  Ni ule uvumilivu katika kutoa huduma yetu [kwa wengine] unaoleta raha nafsini mwetu.  Ni kwa njia ya kufanya kazi kwa taabu, unyenyekevu, bidii, na uaminifu, ndipo usitawi wa Israeli unakuzwa.  Mungu anamsaidia na kumtia nguvu mtu yule anayependa kuifuata njia ile aliyopita Kristo.

     Utakaso si kazi ya dakika moja, saa moja, siku moja, bali ni ya maisha yote ya mtu.  Haupatikani kwa kusikia furaha inayopita upesi moyoni, bali ni matokeo ya kuifia dhambi kila siku, na kuishi kwa ajili ya Kristo kila siku.  Makosa hayawezi kurekebishwa wala matengenezo kufanyika katika tabia kwa kutumia juhudi dhaifu, zinazokatizwa-katizwa [yaani, zisizoendelea bila kukatika kwa maisha yote ya mtu huyo].  Ni kwa juhudi ile tu ya muda mrefu, isiyokubali kushindwa, iliyo na nidhamu kali sana, inayoingia katika pambano kali bila kujihurumia, tutaweza kushinda.  Katika kipindi cha siku moja hatujui pambano linalofuata litakuwa kali jinsi gani.  Kadiri Shetani anavyoendelea kutawala, tutapaswa kuikandamiza [kuitesa] nafsi yetu, na kuzishinda dhambi zile zinazotusonga sana;  kadiri maisha yetu yatakavyoendelea kuwapo, hapatakuwa na mahali pa kusimama, hapatakuwa na kituo[cha kupumzika] tutakachoweza kukifikia na kusema,  Nimekwisha kufika kabisa.  Utakaso ni matokeo ya UTII [kwa Amri Kumi za Mungu] unaoendelea kwa maisha yote ya mtu

     Hakuna hata mmoja miongoni mwa wale Mitume na Manabii aliyepata kudai kwamba hakuwa na dhambi.  Watu wale walioishi karibu sana na Mungu, yaani, watu wale ambao wangekuwa tayari kupoteza maisha yao kuliko kutenda kwa makusudi tendo moja baya, watu wale ambao Mungu amewaheshimu kwa kuwapa nuru ile ya mbinguni na uwezo, wamekiri kwamba walikuwa na asili ya dhambi.  Hawajaliweka tumaini lao katika mwili huu, hawajapata kudai kwamba wao wanayo haki yao wenyewe, bali wameitegemea kabisa kabisa haki ile ya Kristo.

     Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa wote wanaomtazama Kristo.  Kadiri tunavyozidi kumkaribia Yesu, ndivyo tunavyozidi kutambua kwa wazi zaidi usafi [utakatifu] wa tabia yake na kwa wazi zaidi tunauona ubaya wa dhambi uliokithiri, na ndivyo tutakavyozidi kupungua [Yohana 3:30] katika kujikweza wenyewe [yaani, katika kujiona kuwa sisi tu bora kuliko wengine].  Nafsi yetu itazidi kumtafuta Mungu kila wakati, patakuwa na kazi ya kudumu ya kuziungama dhambi zetu mbele zake kwa dhati na kwa majuto, na kwa unyenyekevu wa moyo.  Kwa kila hatua tutakayosonga mbele katika maisha yetu ya Kikristo toba yetu itazidi kuwa na kina zaidi.  Tutakuja kujua kwamba utoshelevu wetu unatoka kwa Kristo peke yake, nasi tutalifanya kuwa letu ungamo hili la Mtume:  “Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, (yaani, ndani ya mwili wangu,) halikai neno jema.”  “Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.”  Warumi 7:18;  Wagalatia 6:14.

     Waacheni malaika wale wanaotunza kumbukumbu zetu waandike historia ya juhudi takatifu na mapambano ya watu wa Mungu;  waacheni waandike kumbukumbu za sala zao;  lakini Mungu wetu asipate kufedheheshwa kwa tamko hili linalotoka katika kinywa cha mwanadamu, lisemalo:  “Mimi sina dhambi kabisa;  Mimi ni mtakatifu.”  Kinywa kilichotakaswa hakitatoa kamwe tamko kama hilo lenye maneno ya kiburi cha makusudi.

     Mtume Paulo alikuwa amenyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu, huko alikuwa ameona   na   kuyasikia   mambo   ambayo   haijuzu   [si   halali]   mwanadamu    ayanene 

[2 Wakorintho 12:1-5, KJV], licha ya hayo, usemi wake usiojitakia makuu ni huu:  “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu;  la!  bali nakaza mwendo.”  Wafilipi 3:12.  Hebu malaika wale wa mbinguni na waandike habari za ushindi wa Paulo katika kupiga vita vile vizuri vya imani.  Hebu mbingu na ishangilie kwa hatua zake thabiti alizokwenda kuelekea mbinguni, na ya kwamba yeye akiwa anaiona mede ya thawabu mbele yake, aliyahesabu mambo yote kuwa kama mavi [Wafilipi 3:8].  Malaika wanafurahi sana kusimulia juu ya ushindi wake, lakini Paulo hajisifu kwa mambo yale [ya kiroho] aliyoyafikia.  Mtazamo wa Paulo unapaswa kuwa ndio mtazamo alio nao kila mfuasi wa Kristo anapokaza mwendo katika pambano lake la kuwania taji ile ya uzima wa milele.

     Wale walio na mwelekeo wa kujisikia kwamba wanayo haja ya kutoa madai ya hali ya juu kuwa wao ni watakatifu, hebu na wajiangalie katika kioo cha Sheria ya Mungu [Amri Kumi].  Wanapoyaona madai yake mapana sana, na kuitambua kazi yake [Sheria hiyo] ya kuyapambanua mawazo na makusudi ya moyo [Ebr. 4:12,13], hawataweza kujisifu sana kuwa hawana dhambi kabisa.  “Tukisema,” asema Yohana, akijihesabu na yeye mwenyewe, “kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewewala kweli haimo mwetu.”  “Tukisema kwamba hatukutenda dhambitwamfanya Yeye kuwa mwongo wala Neno lake halimo mwetu.”  “Tukiziungama dhambi zetu,  Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wetu.”  1 Yohana 1:8,10,9.

     Wapo wale wanaojidai kuwa ni watakatifu, wanaojitangaza kwamba wao ni wa Bwana kabisa, ambao wanadai kwamba wanayo haki ya kuzidai ahadi za Mungu, wakati wao wanakataa kutoa utii wao kwa amri zake [kumi].  Wavunjaji hao wa Sheria [Amri Kumi] wanadai [Mungu awatimizie] kila kitu kilichoahidiwa kwa watoto wa Mungu;  lakini jambo hilo ni kiburi cha makusudi mazima kwa upande wao, kwa maana Yohana anatuambia sisi kwamba upendo wa kweli kwa Mungu utaonekana katika utii wetu kwa Amri zake zote [Kumi].  Haitoshi kuiamini nadharia ya ile kweli, haitoshi kumwamini Kristo, kusadiki kwamba Yesu si laghai, na kwamba dini ya Biblia si hadithi zilizotungwa kwa werevu.  “Yeye asemaye,  Nimemjua [Nimeokoka], wala hazishiki Amri zake [Kumi], alisema Yohana,  “ni MWONGO, wala kweli haimo ndani yake.  Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli.  Katika hili twajua kuwa tumo ndani yake.”  “Naye azishikaye Amri zake [Kumi] hukaa ndani yake, yeye naye ndani yake.”  1 Yohana 2:4,5;  3:24.

     Yohana hakufundisha kwamba wokovu ungeweza kupatikana kwa utii, bali kwamba utii huo ulikuwa tunda la [matokeo ya] imani na upendo.  “Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi [auondoe uvunjaji wa Amri Kumi – 1 Yoh. 3:4, AJKK];”  alisema,  “na dhambi haimo [uvunjaji wa Amri Kumi haumo] ndani yake [Yoh. 15:10].  Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi [havunji Amri Kumi kwa makusudi];  kila atendaye dhambi [kila azivunjaye Amri Kumi] hakumwona yeye, wala hakumtambua.”  1 Yohana 3:5,6.  Tukikaa ndani ya Kristo, upendo wa Mungu hukaa moyoni mwetu, basi, hisia zetu za moyoni, mawazo yetu, na matendo yetu yatapatana na mapenzi ya Mungu [Zab. 40:8;  Mhu. 12:13,14].  Moyo ule uliotakaswa utapatana na Amri Kumi za Sheria ya Mungu [Kut. 20:3-17].

     Wapo wengi ambao, ingawa wanajitahidi kuzitii Amri [Kumi] za Mungu, wana amani au furaha kidogo mno.  Upungufu huo unaoonekana katika maisha yao ni matokeo ya kushindwa kwao kutumia imani.  Wanatembea kana kwamba wamo katika nchi iliyojaa chumvi, na katika nyika kame.  Wanadai kidogo mno [ahadi za Mungu], ambapo wangeweza kudai [wapate kutimiziwa] mengi;  maana hakuna kikomo cha kutimizwa kwa ahadi za Mungu.  Watu kama hao hawauwakilishi vizuri utakaso ule unaokuja kwa njia ya utii kwa ile kweli [Yoh. 17:17;  Zab. 119:142].  Bwana angependezwa kama wana na binti zake wote wangekuwa na furahaamani, na utii.  Kwa kutumia imani, kila upungufu unaoonekana katika tabia unaweza kujaziwa, kila uchafu kutakaswa, kila kosa kusahihishwa, kila uzuri wa tabia kukuzwa.

     Maombi ni njia iliyowekwa na Mbingu ya kupata ushindi katika pambano letu dhidi ya dhambi na katika kuikuza tabia yetu ya Kikristo.  Mivuto mitakatifu inayokuja kama jibu kwa maombi ya imani itafanikiwa kutenda kazi katika moyo wa mwombaji kwa kumpatia yale yote aombayo.  Kwa ajili ya kupewa msamaha wa dhambi, kwa ajili ya kupewa Roho Mtakatifu, kwa tabia ile inayofanana na ya Kristo, kwa ajili ya kupewa hekima na nguvu ili kufanya kazi yake, kwa kipawa cho chote alichotuahidi, tunaweza kuomba;  na ahadi yake ni hii,  “Mtapokea.”

     Ilikuwa ni katika mlima ule, akiwa pamoja na Mungu, Musa alipokiona kiolezo cha jengo lile la ajabu ambalo lilikusudiwa kuwa maskani ya kukaa utukufu wa Mungu.  Ni katika mlima tukiwa pamoja na Mungu  -  katika mahali petu pa faragha pa maombi  -    tunapopaswa kuutafakari mfano ule ulio bora kwa wanadamu. Kwa njia hiyo ya mawasiliano na mbingu, Mungu amejitahidi, katika vizazi vyote, kuonyesha kusudi lake kwa watoto wake, kwa kuwafunulia katika mawazo yao, hatua kwa hatua, mafundisho ya neema yake.  Njia yake ya kutugawia kweli yake imeonyeshwa kwa kielelezo katika maneno haya,  “Kutokea kwake ni yakini kama asubuhi.”  Hosea 6:3.  Ye yote anayejiweka mahali pale Mungu awezapo kumtia nuru, yaani, asongapo mbele, kama ilivyo, kutoka katika utusitusi wa mapambazuko na kuingia katika nuru kamili ya adhuhuri.

     Utakaso wa kweli una maana ya kuwa na upendo mkamilifu, utii kamili, kupatana kabisa na mapenzi ya Mungu.  Tunapaswa kutakaswa kwa Mungu kwa njia ya kuitii ile kweli.  Dhamiri zetu ni lazima zisafishwe na matendo mafu ili tupate kumwabudu Mungu aliye hai.  Hatujawa wakamilifu bado [Wafilipi 3:12-14];  lakini ni haki yetu kuzikata kamba za nafsi na dhambi zetu ambazo zinatufunga, na kukaza mwendo kwenda kwenye ukamilifu.  Uwezekano mkubwa upo ambao kwa huo wote wanaweza kuufikia [ukamilifu], yaani, kukifikia kimo kile cha juu cha utakatifu [Efe. 4:13].

     Sababu inayowafanya wengi katika kizazi hiki cha ulimwengu kushindwa kukaza mwendo katika maisha haya matakatifu inatokana na tafsiri yao ya mapenzi ya Mungu kwamba yanamaanisha kile tu ambacho wao wanataka kufanya.  Wakiwa wanazifuata tamaa zao, wanajisifu mno wenyewe isivyostahili kwamba wao wanapatana kabisa na mapenzi ya Mungu.  Hawa hawana pambano lo lote na nafsi zao.  Kuna wengine ambao kwa wakati fulani wanafanikiwa katika vita yao dhidi ya tamaa yao ya uchoyo [ubinafsi], ya kupenda anasa na raha.  Wao ni wanyofu wa moyo, tena wana bidii, lakini wanachoka kuendelea kujitahidi kwa muda mrefu, wanachoka kufa kila siku, wanachoka kukabiliana na maudhi yasiyokwisha.  Kwao uvivu huonekana kuwa ni kitu cha kutamanika, kuifisha nafsi huonekana kuwa ni kitu cha kuchukiza kwao;  tena wanafumba macho yao yenye usingizi na kuanguka chini ya uwezo wa jaribu linalowakabili badala ya kulipinga.

     Maagizo yale yaliyowekwa katika Neno la Mungu hayaachi nafasi yo yote ya kuridhiana [kupatana] na uovu.  Mwana wa Mungu alidhihirishwa ili apate kuwavuta watu wote kwake.  Hakuja ili kuulaza usingizi ulimwengu, bali kuuonyesha njia ile nyembamba ambayo ni lazima waipitie wale wote wanaotaka kufika kwenye malango yale ya Jiji la Mungu.  Watoto wake ni lazima wafuate kule alikowaongoza njia;  kwa kujitoa mhanga na kujinyima raha au kuacha kujifurahisha wenyewe kwa tamaa zao za mwili kwa gharama yo yote ile na kufanya kazi au kuteswa, ni lazima  waliendeleze pambano lao la kudumu dhidi ya nafsi zao [1Kor. 9:27].

     Sifa kuu mno wanadamu wanayoweza kumletea Mungu ni kuwa mifereji iliyotolewa wakf kwake ambayo anaweza kuitumia katika kufanya kazi yake.  Kwa haraka sana muda unapita kuelekea kwenye umilele.  Hebu na tusizuie kwa Mungu kile ambacho ni chake.  Hebu na tusimkatalie kumpa mali yake.  Hebu na tusimkatalie kumpa kile ambacho, ingawa hakiwezi kutolewa kwake pasipo matendo mema [yanayotendwa kwa neema yake], hakiwezi kuzuiwa kwake bila kujiangamiza wenyewe.  Yeye anaomba mumpe moyo wote;  mpeni;  ni wake, kwa uumbaji na kwa ukombozi wake.  Anaomba mumpe akili zenu;  basi, mpeni;   ni zake.  Anaomba mumpe fedha zenu;  mpeni, ni zake.  “Wala ninyi si mali yenu wenyewe;  maana mlinunuliwa kwa thamani.”  1 Wakorintho 6:19,20.  Mungu anataka asujudiwe na mtu yule aliyetakaswa, aliyejiweka tayari kwa kuitumia imani yake itendayo kazi kwa upendo ili kuweza kumtumikia yeye.  Mbele yetu anatuonyesha kwa kiwango cha juu kile anachotaka sisi tukifikie, yaani, ukamilifu.  Anatutaka sisi kabisa kabisa, na kwa utimilifu kuwa wake [yaani, tumwakilishe] katika ulimwengu huu kama vile yeye alivyo wetu [anavyotuwakilisha] mbele za Mungu.

     “Maana  haya  ndiyo  mapenzi  ya  Mungu,”   kuwahusu  ninyi,  “kutakaswa  kwenu.”  1 Wathesalonike 4:3.  Je!  hayo ni mapenzi yenu pia?  Dhambi zenu zinaweza kuonekana kama milima mbele yenu, lakini ninyi mkiinyenyekeza mioyo yenu na kuziungama dhambi zenu, mkitegemea wema wa Mwokozi wenu aliyesulibiwa na kufufuka, hapo ndipo yeye atawasamehe na kuwasafisha na udhalimu wote.  Mungu anawadai ninyi kuishi kwa kupatana kabisa na Sheria yake [Amri Kumi].  Sheria hiyo [Amri Kumi] ni mwangwi wa sauti yake isemayo kwenu,  Iweni watakatifu zaidi, naam, na mzidi kuwa watakatifu zaidi.  Tamanini kupewa utimilifu wa neema yake Kristo.  Hebu mioyo yenu na ijazwe na shauku kubwa sana ili mpate kuwa na haki yake, kazi ambayo Neno la Mungu linasema kwa mkazo kwamba inaleta amani [moyoni], na matokeo yake ni utulivu na matumaini milele.  

     Kama roho zenu zinamtamani sana Mungu, basi, ninyi mtaweza kuupata utajiri wa neema yake isiyopimika, ambayo itazidi kuongezeka kwenu zaidi na zaidi.  Mtakapotafakari juu ya utajiri huo, utakuwa wenu hasa, nanyi mtaonyesha sifa za kafara ile aliyoitoa Mwokozi wenu, yaani, ulinzi wa haki yake, utimilifu wa hekima yake, na uweza wake wa kuwasimamisha mbele za Baba yake mkiwa “hamna mawaa wala aibu.”  2 Petro 3:14.

 

          E. G. White,  The Acts of the Apostles,  Sura ya 55,  uk. 557-567.

 

ZINGATIA:  Maneno na mafungu ya Biblia yaliyofungiwa ndani ya mabano haya [      ] yameongezwa kwa ufafanuzi tu kwa yule anayetaka kusoma kwa kina au anayeona neno lililotumika pale ni gumu.  Wakati wa kusoma unatakiwa kuyaruka, isipokuwa kama yanasaidia kuikamilisha sentensi hiyo.

Related Information