>Mwanzo >Masomo >Katika roho na nguvu ya Eliya

Katika roho na nguvu ya Eliya

“Katika  Roho  na  Nguvu  Za  Eliya”

 

     Kupitia katika karne ndefu zilizopita tangu wakati ule wa Eliya, kumbukumbu ya kazi yake ya maisha imewatia nguvu na ujasiri wale walioitwa kuitetea haki katikati ya uasi.  Na kwetu sisi, “tuliofikiliwa na miisho ya zamani” hizi (1 Wakorintho 10:11), ina maana ya pekee.  Historia inajirudia yenyewe.  Ulimwengu leo unao akina Ahabu wake na akina Yezebeli wake.  Kizazi cha sasa ni kimoja ambacho kinaabudu sanamu, ni sawa kabisa na kile alichoishi Eliya.  Hakuna madhabahu inayoweza kuonekana kwa macho;  huenda pasiwepo na sanamu yo yote ambayo jicho linaweza kuitazama, lakini bado maelfu wanaifuata miungu ya ulimwengu huu  -  yaani, wanafuata utajiri, sifa, anasa, na hadithi za uongo zinazopendeza ambazo zinamruhusu mwanadamu kufuata mielekeo ya moyo wake ambao haujazaliwa mara ya pili.  Watu wengi sana wana dhana potofu kuhusu Mungu na sifa zake, nao, kusema kweli, wanamtumikia mungu wa uongo kama vile walivyofanya wale waliomwabudu Baali.  Wengi, hata miongoni mwa wale wanaojiita Wakristo, wamejifungamanisha wenyewe na mivuto ile inayompinga Mungu na kweli yake bila [kuonyesha] badiliko lo lote.  Hivyo ndivyo wanavyoongozwa kumpa Mungu kisogo na kumtukuza mwanadamu.

     Roho iliyopo kwa wakati wetu huu ni ya ukafiri na uasi  -  roho inayokiri kwamba imeipokea nuru ati kwa sababu tu inaijua kweli hiyo, lakini kusema kweli huo ni upofu kabisa uliojaa kiburi cha makusudi.  Nadharia za wanadamu hutukuzwa na kuwekwa mahali pale anapostahili kuwapo Mungu na Sheria yake [Amri Kumi].  Shetani huwashawishi wanaume na wanawake wasitii, kwa ahadi kwamba wasipotii watakuwa wamefunguliwa na kupata uhuru wao utakaowafanya kuwa kama miungu.  Roho ya upinzani kwa Neno la Mungu lililo wazi huonekana, yaani, roho ile ya kuitukuza na kuiabudu hekima ya kibinadamu zaidi ya ufunuo wa Mungu.  Watu wameiachilia mno mioyo yao kutiwa giza  na kuchanganyikiwa kwa kuzifuata desturi na mambo ya ulimwengu huu hata wanaonekana kana kwamba wamepoteza uwezo wao wote wa kupambanua kati ya nuru na giza, kweli na uongo.  Mpaka hapo wao huwa wameiacha njia ile sahihi kiasi kwamba wanayaona maoni machache ya wale waitwao wana-falsafa kuwa ni ya kuaminika kuliko kweli zile za Biblia.  Kusihi kote na ahadi za Neno la Mungu, vitisho vyake dhidi  ya uasi na ibada ya sanamu  -  mambo hayo huonekana kwao kama hayana uwezo wo wote wa kuilainisha mioyo yao.  Imani kama ile iliyomsukuma Paulo, Petro, na Yohana wanaiona kuwa imepitwa na wakati, ni fumbo kwao, na haifai kwa watu wa kisasa wenye ujuzi na akili nyingi.

     Hapo mwanzo, Mungu aliwapa wanadamu Sheria yake [Amri Kumi] kama njia ya kupatia furaha na uzima wa milele.  Tumaini pekee la Shetani la kulizuia kusudi la Mungu ni katika kuwashawishi wanaume na wanawake wasiitii Sheria hiyo [Amri Kumi], na juhudi yake inayoendelea daima imekuwa ni ile ya kupotosha mafundisho yake [hiyo Sheria] na kuifanya ionekane haina maana sana.  Ustadi wake mkubwa sana ni ule wa kufanya jaribio lake la kuibadili Sheria yenyewe [Amri Kumi], ili kuwafanya watu kuzivunja amri zake huku wakidai kwamba wanaitunza Sheria yake [Amri Kumi].

     Mwandishi mmoja amelilinganisha jaribio hilo la kuibadili Sheria ya Mungu [Amri Kumi] na utundu wa zamani wa kufanya mchezo wa kukigeuza kibao kilichowekwa mahali ambapo barabara mbili zinakutana ili kuonyesha njia na kukielekeza upande usiokuwa wenyewe.  Kitendo hicho mara nyingi kilileta mfadhaiko na shida kubwa.

     Kibao cha kuonyesha njia kiliwekwa na Mungu kwa wale wanaosafiri katika dunia hii.  Mkono mmoja wa kibao hicho ulionyesha utii wa hiari kwa Muumbaji kama ndiyo barabara iendayo kwenye furaha kuu na uzima wa milele, wakati mkono ule mwingine ulionyesha uasi [uvunjaji wa Amri Kumi] kama ndiyo njia iendayo kwenye huzuni kubwa na mauti.  Njia iendayo kwenye furaha ilielezwa waziwazi kama vile ilivyoelezwa njia ile iliyokwenda kwenye mji wa makimbilio katika kipindi kile cha Wayahudi.  Lakini katika saa ile ya uovu kwa taifa letu la kibinadamu, adui yule mkuu wa mema yote alikigeuza kibao kile, na watu wengi sana wamepotea njia.

     Kupitia kwa Musa, Bwana aliwaagiza Waisraeli, akasema:  “Hakika mtazishika Sabato [Jumamosi] zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote;  ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi.  Basi mtaishika hiyo Sabato [Jumamosi];  kwa kuwa ni takatifu kwenu;  kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa;  kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi … katika siku ya Sabato [Jumamosi], hakika yake atauawa.  Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato [Jumamosi], kuiangalia sana hiyo Sabato [Jumamosi] katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele.  Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele;  kwani kwa siku sita BWANA alifanya mbingu na nchi, akastarehe kwa siku ya saba [Jumamosi] na kupumzika.”  Kutoka 31:13-17.

     Kwa  maneno  hayo  Bwana alieleza waziwazi kwamba utii ni njia ya kuingilia katika lile Jiji la Mungu;  lakini yule mtu wa dhambi [aliyeivunja Sheria kwa kuibadili – 

2The. 2:1-4] amekigeuza kibao kinachoonyesha njia na kukielekeza upande usiokuwa wenyewe.  Ameiweka sabato ya uongo [Jumapili] na kuwafanya wanaume na wanawake kufikiri kwamba kule kupumzika kwao katika siku hiyo [ya Jumapili] walikuwa wanaitii amri ya Muumbaji wao [Kut. 20:8-11].

     Mungu ametangaza kwamba siku ya saba [Jumamosi] ni Sabato yake Bwana.  Wakati ule “mbingu na nchi zi[lipo]malizika,” aliitukuza siku hiyo [ya Jumamosi] kama kumbukumbu ya kazi yake ya uumbaji.  Akastarehe siku ile ya saba “akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya,”  “Mungu akaibarikia siku ya saba [Jumamosi], akaitakasa.”  Mwanzo 2:1-3.

     Wakati ule wa Kutoka toka Misri, amri hiyo ya Sabato [Jumamosi] ilionyeshwa waziwazi kabisa mbele ya watu wale wa Mungu.  Walipokuwa wangali bado utumwani, wasimamizi wao wa kazi walikuwa wamejaribu kuwalazimisha kufanya kazi siku ya Sabato [Jumamosi] kwa kuwaongezea kazi nyingi sana kuliko ile iliyotakiwa kila juma.  Tena na tena hali ya kazi yao ikafanywa kuwa ngumu zaidi na ya kusimamiwa kwa ukali.  Lakini Waisraeli wale waliokolewa kutoka utumwani na kuletwa mahali ambapo wangeweza kuzitunza amri zote [kumi] za Yehova bila kusumbuliwa.  Pale Sinai Sheria [Amri Kumi] ilinenwa;  na nakala yake, juu ya mbao zile mbili za mawe, ili“andikwa kwa chanda (kidole) cha Mungu” na kukabidhiwa kwa Musa.  Kutoka 31:18.  Na karibu kipindi chote cha miaka ile arobaini cha kutangatanga jangwani kwa Waisraeli, walikumbushwa daima juu ya siku hiyo ya kupumzika iliyowekwa na Mungu, kwa njia ya kuizuia mana kila siku ya saba [Jumamosi] na kukitunza kwa mwujiza ili kisioze chakula kile kilichokusanywa maradufu ambacho kilidondoka siku ile ya Maandalio [Ijumaa].

     Kabla  hawajaingia  katika  Nchi  ile  ya  Ahadi,  Waisraeli  wale  walionywa na Musa

ku“ishik[a] siku ya Sabato [Jumamosi] [k]uitakas[a].”  Kumbukumbu la Torati 5:12.  Bwana alikusudia kwamba kwa kuitunza kwa uaminifu amri ya Sabato [Jumamosi], Israeli wangekumbushwa daima juu ya uwajibikaji wao kwake kama Muumbaji na Mkombozi wao.  Wakati ambapo wao wangekuwa wanaitunza Sabato [Jumamosi] kama inavyotakiwa, isingekuwako ibada ya sanamu;  lakini kama madai ya Sheria hiyo ya Amri Kumi yangewekwa kando kwa kusema kwamba hayamfungi mtu ye yote, basi, Muumbaji huyo angeweza kusahauliwa, na wanadamu wangeweza kuiabudu miungu mingine.  “Tena naliwapa Sabato [Jumamosi] zangu,”  Mungu alitangaza, “ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, BWANA, ndimi niwatakasaye.”  Lakini “walizikataa hukumu zangu, wala hawakuenda katika amri zangu [kumi], wakazitia unajisi Sabato [Jumamosi] zangu, kwa maana mioyo yao iliandama vinyago vyao.”  Na katika ombi lake la kuwataka wamrudie yeye, aliyageuza upya mawazo yao kuangalia umuhimu wa kuitakasa Sabato:  “Mimi ni BWANA, Mungu wenu,”  akasema, “endeni katika amri zangu [kumi], na kuzitenda;  zitakaseni Sabato [Jumamosi] zangu;  nazo zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa ndimi BWANA, Mungu wenu.”  Ezekieli 20:12,16,19,20.

     Katika kuwakumbusha Yuda juu ya dhambi zao zilizowafanya wapelekwe utumwani Babeli, Bwana aliwatangazia hivi:  “Umezitia unajisi Sabato [Jumamosi] zangu.”  “Kwa sababu hiyo nimemwaga ghadhabu yangu juu yao;  nimewateketeza kwa moto wa hasira yangu;  nami nimeileta njia yao wenyewe juu ya vichwa vyao.”  Ezekieli 22:8,31.

     Wakati  ule  wa  kujengwa  upya  kwa  Yerusalemu,  katika  siku  za  Nehemia, uvunjaji  wa  Sabato  [Jumamosi]  ulikutana  na hoja kali,  “Je!  sivyo hivyo walivyofanya  baba  zenu;   na  Mungu  wetu,   je!   hakuyaleta  mabaya  haya  yote juu ya mji huu?  nanyi hata hivyo mwazidi kuleta ghadhabu juu ya Israeli kwa kuinajisi Sabato [Jumamosi]!”   Nehemia 13:18.

     Kristo, wakati wa kazi yake hapa duniani, aliyakazia madai ya Sabato [Jumamosi] ambayo yanawafunga wanadamu wote;  katika mafundisho yake yote alionyesha heshima kwa siku hiyo aliyoiweka yeye mwenyewe.  Katika siku zake Sabato [Jumamosi] ilikuwa imetumiwa vibaya sana kiasi kwamba utunzaji wake ulidhihirisha tabia ya wanadamu ya uchoyo na utumiaji nguvu kuliko tabia ile ya Mungu.  Kristo aliyaweka kando mafundisho ya uongo ambayo kwayo wale waliodai kwamba wanamjua Mungu walikuwa wamemwakilisha vibaya.  Ingawa Marabi walimfuatilia kwa chuki isiyokuwa na huruma, yeye hakuonekana hata kidogo kufuata matakwa yao, bali alisonga mbele kuitunza Sabato kulingana na Sheria ya Mungu [Amri Kumi].         

     Kwa kutumia lugha isiyoweza kukosewa alitoa ushuhuda wake ulioonyesha kwamba yeye anaijali Sheria ile ya Yehova [Amri Kumi].  “Msidhani [wengi mno leo wanadhani] ya kuwa nalikuja kuitangua torati [Sheria] au manabii;”  akasema, “sikuja kutangua [kuifutilia mbali], bali kutimiliza [kuitekeleza].  Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka [bado zipo], yodi moja [,] wala nukta moja [.] HAITAONDOKA hata yote yatimie [yaani, mpaka hapo mbingu na nchi zitakapoondoka].  Basi [kwa hiyo] mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo [Yak.2:10-12], na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa [mnyonge hataingia – Ufu.21:27] katika ufalme wa mbinguni;  bali mtu ATAKAYEZITENDA [Amri Kumi] NA KUZIFUNDISHA, huyo ataitwa mkubwa [mtawala/mfalme – Ufu.20:4;  Dan. 7:27] katika ufalme wa mbinguni.”  Mathayo 5:17-19.

     Katika kipindi hiki cha Ukristo, adui huyo mku u wa furaha ya mwanadamu ameifanya Sabato [Jumamosi] ya amri ya nne [Kut. 20:8-11] kuwa lengo la mashambulio yake maalum.  Shetani asema,  “Nitafanya kazi yangu ili kuyapinga makusudi ya Mungu.  Nitawapa wafuasi wangu uwezo wa kuiweka kando kumbukumbu hiyo ya Mungu, yaani, Sabato ya siku hiyo ya saba [Jumamosi].  Kwa njia hiyo nitauonyesha ulimwengu ya kuwa siku ile iliyotakaswa na kubarikiwa na Mungu [Jumamosi] imebadilishwa.  Siku hiyo haitabaki katika mawazo ya watu.  Nitaifutilia mbali kumbukumbu yake.  Mahali pake nitaiweka siku [ya Jumapili] ambayo haitambuliwi na Mungu, yaani, siku ambayo haiwezi kuwa ishara kati ya Mungu na watu wake.  Nitawaongoza wale wanaoikubali siku hii [ya Jumapili] kuweka juu yake utakatifu ule aliouweka Mungu katika siku ile ya saba [Jumamosi].

     “Kupitia kwa makamu wangu [mtu yule wa dhambi – 2The. 2:3,4], nitajitukuza mimi mwenyewe.  Siku ya kwanza [Jumapili] itatukuzwa, na Ulimwengu wa Kiprotestanti utaipokea sabato hiyo ya uongo [Jumapili] kama ndiyo siku halali [ya ibada].  Nitayadhibiti mawazo ya watu walio chini ya uwezo wangu kiasi cha kuifanya Sabato ya Mungu [Jumamosi] kuwa ishara ya uasi kwa wenye mamlaka [watawala] wa dunia hii.  Amri za wanadamu zitakuwa kali mno hata wanaume na wanawake hawatathubutu kuitunza Sabato ya siku ya saba [Jumamosi].  Kwa hofu ya kukosa chakula na mavazi, watajiunga na ulimwengu katika kuivunja Sheria ya Mungu [Amri Kumi].  Dunia yote itakuwa chini ya utawala wangu” [asema Shetani].

     Kwa njia ya kuiweka sabato ya uongo [Jumapili], yule adui alifikiria kubadili majira na sheria [Amri Kumi].  Lakini, je!  hivi amefanikiwa kweli kuibadili Sheria ya Mungu [Amri Kumi]?  Maneno ya Sura ya Thelathini na Moja ya kitabu cha Kutoka ndilo jibu lake.  Yule ambaye ni yeye yule [yaani, habadiliki kamwe] jana, leo, na hata milele [Ebr. 13:8], ametangaza hivi kuhusu siku ya saba [Jumamosi]:  “Ni ishara …  milele.”  Kutoka 31:13,17.  Kibao kinachoonyesha njia kimebadilishwa na kuonyesha njia ambayo siyo yenyewe, lakini Mungu hajabadilika.  Yeye  bado ni Mungu Mwenyezi wa Israeli.  “Tazama, mataifa ni kama tone la maji katika ndoo, huhesabiwa kuwa kama ni kitu kidogo sana.  Lebanoni nayo hautoshi kwa kuni, wala wanyama wake hawatoshi kwa kafara.  Mataifa yote huwa kama si kitu mbele zake;  huhesabiwa kwake kuwa duni ya si kitu, na ubatili.”  Isaya 40:15-17.  Naye ana wivu kwa ajili ya Sheria yake [Amri Kumi] sasa kama alivyokuwa nao katika siku za Ahabu na Eliya.

     Lakini Sheria ile [Amri Kumi] hudharauliwa jinsi gani!  Angalia ulimwengu leo umefanya uasi waziwazi dhidi ya Mungu.  Hiki, kusema kweli, ni kizazi kikaidi [kilichoasi], kimejaa utovu wa shukrani, kinashika dini kama desturi tu, ni kinafiki, kimejaa kiburi, na uasi.  Watu wanaidharau Biblia na kuichukia kweli.  Yesu anaona Sheria yake [Amri Kumi] ikikataliwa, upendo wake ukidharauliwa, na mabalozi [wajumbe] wake wakitendewa kwa ubaridi [yaani, bila kuwajali].  Amenena kwa njia ya rehema zake, lakini hizo hazijapokelewa;  amenena kwa maonyo, lakini hayo hayajazingatiwa.  Nyua za hekalu la moyo wa mwanadamu zimegeuzwa na kuwa mahali pa biashara haramu. Uchoyo, wivu, kiburi, kijicho  -  vyote hivyo vinatunzwa humo.

     Wengi hawasiti kulikenulia meno Neno la Mungu.  Wale wanaoliamini Neno hilo kama linavyosomeka wanakuwa ni watu wa kudhihakiwa.  Kuna dharau inayozidi kuongezeka kuhusu utii kwa sheria [za nchi], ambayo inaweza kufuatiliwa moja kwa moja hadi kwenye uvunjaji wa amri [kumi] za Yehova ambazo ziko dhahiri.  Vitendo vya kutumia nguvu na uhalifu ni matokeo ya kugeukia kando ya njia ile ya utii.  Angalia ufukara (ukata) na dhiki waliyo nayo watu wengi wanaoabudu kwenye madhabahu ya sanamu, ambao wanafanya kazi bure kutafuta furaha na amani.

     Angalia kule kutokuijali amri ya Sabato [Jumamosi] kulivyoenea karibu ulimwenguni kote.  Angalia pia kukufuru bila kuwa na hofu kwa wale ambao, wakati wanatunga sheria za kuulinda utakatifu unaodhaniwa-dhaniwa tu wa siku ya kwanza ya juma [Jumapili], na wakati uo huo wanatunga sheria zinazohalalisha biashara ya vileo.  Wakiwa ni wenye hekima kuliko kile kilichoandikwa [katika Biblia], wanajaribu kuzilazimisha dhamiri za watu, wakati wao wanaunga mkono uovu huo [vileo] unaowafanya kuwa kama wanyama wakali na kuwaangamiza viumbe wale walioumbwa kwa sura ya Mungu.  Ni Shetani mwenyewe anayechochea utungaji wa sheria kama hizo.  Anajua fika kwamba laana ya Mungu itawakalia wale wanaozitukuza sheria zilizotungwa na wanadamu kuliko ile ya Mungu, naye anafanya kwa uwezo wake wote kuwaongoza wanadamu katika njia ile pana ambayo mwisho wake ni maangamizi.

     Kwa muda mrefu mno wanadamu wameyaabudu maoni ya wanadamu na mambo yaliyowekwa na wanadamu kiasi kwamba karibu ulimwengu mzima unaziandama sanamu.  Na yule aliyejaribu kuibadili Sheria ya Mungu [Amri Kumi] anatumia kila aina ya udanganyifu ili kuwashawishi wanaume na wanawake kujipanga kinyume na Mungu na kinyume na ishara yake [Sabato/Jumamosi] ambayo inawatambulisha wenye haki.  Lakini Bwana hatavumilia kuiacha Sheria yake [Amri Kumi] ikiwa inavunjwa na kudharauliwa sikuzote bila ya watu kuwa na hofu kwamba wataadhibiwa.  Wakati unakuja ambapo “macho ya mwanadamu yaliyoinuka yatashushwa chini, na kiburi cha mwanadamu kitainamishwa, naye BWANA, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo.”  Isaya 2:11.  Kuwa na mashaka kunaweza kuyachukulia madai ya Sheria ya Mungu [Amri Kumi] kama mzaha, dhihaka, na kuyakataa kabisa.  Roho ya kuipenda dunia inaweza kuwanajisi wengi na kuwatawala wachache, kazi ya Mungu inaweza kuendelea tu kwa juhudi kubwa na kwa kuendelea daima kujitolea mhanga, lakini mwisho wake kweli itashinda vibaya sana.

     Katika kufungwa kwa kazi ya Mungu duniani, kanuni ya Sheria yake [Amri Kumi] itainuliwa tena juu.  Dini ile ya uongo inaweza kuendelea kuwapo, uovu unaweza kuzidi sana, upendo wa wengi unaweza kupoa, msalaba wa Kalvari unaweza kusahauliwa, na giza, kama kengele ya kifo, linaweza kutanda juu ya dunia hii;  jeshi lote la mkondo ule unaopendwa na watu wengi linaweza kuelekezwa dhidi ya ile kweli;  njama baada ya njama inaweza kufanywa ili kuwashinda watu wa Mungu;  lakini katika saa ile ya hatari kubwa mno Mungu yule wa Eliya atawainua wajumbe wake wa kibinadamu ili kuupeleka ujumbe wake ambao hautaweza kunyamazishwa.  Katika miji ya nchi iliyojaa watu wengi, na mahali kule ambako watu wamekwenda mbali mno katika kunena maneno kinyume cha yule Aliye Juu, sauti ya kemeo kali itasikika.  Kwa ujasiri watu wale walioteuliwa na Mungu watausuta hadharani Muungano wa Makanisa [ulioungana] na Ulimwengu huu.  Kwa bidii kubwa watawaita wanaume na wanawake ili wauachilie mbali utunzaji wa siku ile iliyowekwa na wanadamu [Jumapili] na [mahali pake] kuitunza Sabato ya kweli [Jumamosi].  “Mcheni Mungu, na kumtukuza,”  watatangaza kwa  kila  taifa;  “kwa maana saa ya hukumu yake imekuja.  Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji [kwa kuishika Sabato/Jumamosi - Kut. 20:8-11]….  Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama [mtu huyo wa dhambi – 2The. 2:3,4] na sanamu yake [Uprotestanti Asi uliovaa kofia mbili kama mnyama], na kuipokea chapa (alama) katika kipaji cha uso wake [kwa kuendelea kwa makusudi kuabudu siku ya Jumapili], au katika mkono wake, yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu [Mapigo saba – Ufu. 15:1; 16:1-21] iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji.”  Ufunuo 14:7-10.

     Mungu hatalivunja agano lake, wala hatalibadili neno lililotoka midomoni mwake.  Neno lake litasimama imara milele bila kubadilika kama kilivyo kiti chake cha enzi.  Wakati wa hukumu agano hilo litaletwa, likiwa limeandikwa waziwazi kwa kidole chake Mungu, na ulimwengu wote utashtakiwa na kusimama kizimbani katika hukumu ya Mungu mwenye haki kupokea hukumu yao.

     Leo, kama katika siku zile za Eliya, mstari wa katikati unaowagawa watu wale wanaozishika amri [kumi] za Mungu na wale wanaoiabudu miungu ya uongo, umechorwa na uko wazi.  “Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini?”  Eliya akapiga kelele;  “BWANA akiwa ndiye Mungu, mfuateni;  bali ikiwa Baali ni Mungu, haya!  mfuateni yeye.”  1 Wafalme 18:21.  Na ujumbe wa leo ni huu:  “Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu [Muungano wa Makanisa ulioungana na Dunia];…  Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.  Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake.”  Ufunuo 18:2,4,5.

     Wakati hauko mbali sana litakapokuja jaribio hilo kwa kila mtu [Ufu. 3:10].  Utunzaji wa sabato hiyo ya uongo [Jumapili] utalazimishwa juu yetu.  Pambano lenyewe litakuwa juu ya Amri [Kumi] za Mungu [Kut. 20:8-11;  Yak. 2:10-12] na amri za wanadamu.  Wale ambao wamekuwa wakijisalimisha hatua kwa hatua kuyatii matakwa ya ulimwengu huu na kuzifuata desturi za ulimwengu huu, wakati ule wataona ni afadhali kujisalimisha kwa mamlaka [tawala] zitakazokuwako kuliko kujiweka wenyewe chini ya dhihaka, matusi, tishio la kufungwa, na mauti.  Wakati ule dhahabu ndipo itatenganishwa na mavi yake [yaani, takataka].  Utauwa wa kweli utaonekana wazi na kutofautishwa na ule mwonekano wake na unafiki.  Nyota nyingi tulizozitamani sana kwa mng’aro wake, wakati ule zitazimika gizani.  Wale waliojitwalia mapambo ya patakatifu, lakini ambao hawajavikwa haki ya Kristo, wakati ule wataonekana katika aibu ya uchi wao.

     Miongoni mwa wakazi wa dunia hii, waliotawanyika katika kila nchi, wamo wale ambao hawajapata kupiga goti kwa Baali.  Kama nyota za mbinguni, ambazo huonekana wakati wa usiku tu, hao walio waaminifu watang’aa wakati ule giza [la ujinga wa kutokumjua Mungu] litakapoifunika dunia hii na giza kuu litakapowafunika watu.  Katika Afrika ya kishenzi [kipagani], katika nchi za Kikatoliki za Ulaya na Amerika Kusini, katika nchi ya China, katika nchi ya India, katika visiwa vya baharini, na katika kona zote za dunia zenye giza, Mungu amejiwekea akiba ya wateule wake ambao watajitokeza na kung’aa katikati ya giza, wakiuonyesha waziwazi ulimwengu huu ulioasi uwezo ule unaobadili tabia zao utokanao na utii wao kwa Sheria yake [Amri Kumi].  Hata sasa wanaendelea kujitokeza katika kila taifa, miongoni mwa kila lugha na kabila;  na katika saa ile ya uasi mkuu mno juhudi kuu za Shetani zitakapotumika ili kuwafanya [kuwalazimisha] “wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa,” kupokea, chini ya tishio la adhabu ya kifo, alama ya utii wao kwa siku ya kupumzika ya uongo [Jumapili], ndipo waaminifu hao walio “bila lawama na wapole, wana wa Mungu, wasioshutumiwa,”  watakapong’aa “kama mianga katika ulimwengu.”  Ufunuo 13:16;  Wafilipi 2:15, KJV.  Kadiri usiku utakavyozidi kuwa na giza nene zaidi, ndivyo kadiri watakavyozidi kung’aa sana.

     Ingekuwa ni kazi ya ajabu jinsi gani ambayo Eliya angekuwa amefanya kama angeweza kuwahesabu Israeli wakati ule hukumu za Mungu zilipokuwa zinawaangukia watu wale waliorudi nyuma!  Yeye aliweza kumhesabu mtu mmoja tu upande wa Bwana.  Lakini basi, yeye aliposema,  “Nami nimesalia, mimi peke yangu;  nao wanitafuta roho yangu waiondoe,”  neno la Mungu likamshtua, aliposema:  “Pamoja na hayo ni[me]jisazia katika Israeli watu elfu saba, kila goti lisilomwinamia Baali.”  1 Wafalme 19:14,18, KJV.

     Basi, na asiwepo leo mtu ye yote anayejaribu kuwahesabu Israeli, ila kila mmoja na awe na moyo wa nyama, moyo uliojaa upendo na huruma, moyo kama huo, unaofanana na Kristo, utokao na kwenda nje kufanya kazi ya kuuokoa ulimwengu huu uliopotea.

 

     E. G. White,  “In the Spirit and Power of Elias,” -  From Prophets and Kings, Sura ya 14, uk. 177-189.

 

ZINGATIA:  Maneno na mafungu ya Biblia yaliyofungiwa ndani ya mabano haya [     ] yameongezwa kwa ufafanuzi tu kwa yule anayetaka kusoma kwa kina au anayeona neno lililotumika pale ni gumu.  Wakati wa kusoma unatakiwa kuyaruka, isipokuwa kama yanasaidia kuikamilisha sentensi hiyo.