Washindani wawili wenye nguvu
WASHINDANI WAWILI WENYE NGUVU
Japokuwa kilele cha pambano hili kuu kitafikiwa mwishoni kabisa wa historia ya mwanadamu wakati ambapo dunia yote itakuwa imegawanyika katika makambi mawili yanayopingana, pambano hili kati ya Kristo na Shetani limekuwa likiendelea kwa karibu miaka 6000. Lilianza mbinguni kutokana na uasi wa Lusifa dhidi ya utawala wa Mungu wa ulimwengu wote. Kisa cha malaika huyo mzuri aliyetamani cheo cha Mungu Mwenyezi kimefunuliwa katika Maandiko ya manabii kadhaa wa Agano la Kale. Isaya asema hivi kumhusu kiumbe huyo mwenye utukufu: "Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri [Lusifa], mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, NITAFANANA NA YEYE ALIYE JUU." Isaya 14:12-14.
Mbegu za uasi wa malaika huyo kiongozi, uliojaa ubinafsi, zikaenea kwa kasi sana na kuathiri utiifu wa malaika wale wengine. Mara hiyo theluthi moja ya jeshi lile la mbinguni ikawa imejiunga na kutoridhika kwa Lusifa, na pambano lile kuu likawa njiani ----- pambano ambalo lingeendelea kwa ukali sana kwa zaidi ya miaka 6000, na ambalo hatimaye lingetaka uamuzi wa kila kiumbe kilicho hai mbinguni na duniani.
Matokeo ya mara moja ya kutopatana yakawa vita mbinguni ambayo ilifikia kilele chake kwa kumfukuza kabisa Lusifa toka mbele zake Mungu na mbele ya malaika wake watiifu. Yohana analieleza jambo hilo kwa njia hii, "Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule Joka, yule Joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule Joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote, akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye." Ufunuo 12:7-9.
Malaika yule aliyeanguka hakuweza tena kujulikana kama Lusifa, jina lililomaanisha "nyota ya alfajiri" bali Shetani, likimaanisha "adui." Sasa pambano likawa limehamishwa toka mbinguni na kuja chini duniani. Hapa litaendelea mpaka litakapofikia mwisho wake mbaya sana kwa kuwagawa watu wa dunia hii kuwa upande wa au kinyume na Amri za Mungu. Kama vile pambano hili lilivyoanzishwa kwa uasi dhidi ya mamlaka ya Mungu, ndivyo litakavyokwisha kwa watu kukataa katakata mamlaka Yake yaliyowekwa katika Sheria ya Serikali Yake.
Shetani amekuwapo hapa pamoja na malaika zake waovu tangu wakati ule alipofukuzwa toka kwenye mwanga. Kwa hila yake ya kishetani amefanya majaribio ya njia mbalimbali za kupigana vita dhidi ya Mungu na Mpango wake kwa ulimwengu huu. Kwa kutumia njia mbalimbali za siri zenye kudhuru ameendelea na juhudi zake ili kuipindua mamlaka ya Mungu. Kusudi la kijitabu hiki ni kuonyesha kwa wazi mashambulio yake imara ambayo yamekwisha fanywa, na yanayofanywa na Shetani dhidi ya misingi ya ile Kweli.
Kila kizazi kimeshuhudia onyesho jipya la nguvu ile ya uovu katika vita yake bila kuchoka dhidi ya programu ile ya Mbinguni ya kuuokoa ulimwengu huu. Sura ya mwisho ya upinzani huu wa adui itakuwa ni ile ya Mnyama wa Ufunuo 13. Mamlaka ile ya bandia [uongo] itasimamishwa kupambana vikali sana na Amri za Mungu. Ulimwengu wote utatakiwa KUCHAGUA upande huu au ule. Muungano huo wa [nguvu za] uovu utajiimarisha kwa pambano lile la mwisho linalohusu utii wa wakazi wa ulimwengu huu. Mambo [yote] yatakuwa yamewekwa wazi, na hakuna hata mmoja ambaye hatachagua upande wo wote. UTII KWA MUNGU au KWA SHETANI, kama alivyodhihirishwa katika mamlaka ile ya Mnyama, utakuwa ndiyo nafasi ya pekee kwa mwanadamu ya kuchagua kati ya mambo mawili yaliyo mbele yake.