>Mwanzo >Soma Vitabu >joka na mwanamke >Joka na mwanamke-Sura ya kwanza >Ni Suala la kufa na kupona

Ni Suala la kufa na kupona

NI SUALA LA KUFA NA KUPONA

 

 Sasa, tukiwa tumepata maelezo machache ya kihistoria ya nyuma ya hao wanaopambana, hebu na tuangalie kwa karibu zaidi mpangilio wa Biblia kuhusu pambano hili la mwisho la mkataa [kuamua mshindi ni nani] katika pambano lile kuu [lililoanza mbinguni]. Tafadhali zingatia ya kwamba Mnyama wa Ufunuo 13 anawakilisha mamlaka kubwa sana ya MPINGA KRISTO ambayo inajaribu kumwondoa Mungu kabisa. Hapa pana maelezo ya mamlaka ile katika lugha ya Ufunuo 13:1-7 [Toleo la King James], "Nami nikasimama juu ya mchanga wa bahari, kisha nikaona Mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba [taji] kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru. Na yule Mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, YULE JOKA AKAMPA NGUVU ZAKE NA KITI CHAKE CHA ENZI NA UWEZO MWINGI. Nikaona kimoja cha vichwa vyake kana kwamba kimetiwa jeraha la mauti, na pigo lake la mauti likapona. Dunia yote ikamstaajabia Mnyama yule. Wakamsujudu yule Joka kwa sababu alimpa huyo Mnyama uwezo wake; nao wakamsujudu yule Mnyama wakisema, Ni nani afananaye na Mnyama huyu? Tena ni nani awezaye kufanya vita naye? Naye akapewa kinywa cha kunena maneno makuu, ya makufuru.

Akapewa uwezo wa kufanya kazi yake MIEZI AROBAINI NA MIWILI. Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni. Tena akapewa KUFANYA VITA NA WATAKATIFU NA KUWASHINDA, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa."

 Hapa hatuwezi kushindwa kuuona ukubwa usio na kifani wa upinzani huu dhidi ya Mungu na dhidi ya wale wanaomfuata. Baadaye katika sura hii hii, tutasoma kwamba mamlaka hii ya Mnyama itakuwa na ushawishi mkubwa sana juu ya dunia nzima, kiasi cha kuwafanya wanadamu kupokea alama [chapa] katika vipaji vya nyuso zao au katika mkono wao [wa kuume]. (Ufunuo 13:16). Mwishoni, wale walio na alama hiyo WATATESWA KWA GHADHABU YA MUNGU ISIYOCHANGANYWA NA MAJI kama ilivyoelezwa katika Ufunuo 14:9,10. Ghadhabu ya Mungu imefafanuliwa zaidi katika Ufunuo 15:1 kwa maneno haya, "Malaika saba wenye MAPIGO SABA YA MWISHO; maana katika hayo GHADHABU YA MUNGU imetimia."

 Hali ya kutisha ya mapigo hayo na maumivu makali mno watakayopata wale wanaoipokea chapa [alama] ya Mnyama yamewekwa wazi katika sura ile ya kumi na sita ya Ufunuo. Hatutaongea kirefu juu yake kwa wakati huu, ila na tujikumbushe wenyewe ya kwamba jambo hili litahusu uzima wa milele au mauti kwa wote. Ni kwa bidii ilioje, basi, tungetafuta sana kuelewa Mnyama huyo anawakilisha kitu gani, na jinsi tunavyoweza kuikwepa chapa ile. Pasiwe na kubahatisha au kukisia ko kote juu ya somo hili la maana sana. Yatupasa kujua kabisa hatari iko wapi, na jinsi gani tunaweza kuikwepa.

 Mkristo wa kawaida hajapata hata kusikia juu ya umuhimu wa somo hili [kwa maisha yake ya milele]. Hana wazo hata kidogo juu ya Mnyama huyo wala chapa yake, japokuwa maisha yake ya milele yanategemea jambo hilo. Makundi na makundi ya wahubiri wanawafariji watu katika UJINGA wao kuhusu suala hili. Wanasema, "Usiwe na wasiwasi wo wote juu ya Mnyama huyo. Ni jambo gumu sana kulielewa. Mradi tu wewe uzidi kumpenda Bwana utakuwa salama. Huwezi kujua kwa kweli Mnyama huyo ni nani." Sikiliza! Je, Mungu anaweza kutuonya sisi juu ya Mnyama huyo wa kutisha ----- na kisha atuambie ya kwamba haiwezekani kujua huyo ni nani? Je, angeweza kutuambia, "Mtatupwa katika ziwa la moto kama mnayo chapa yake, ila sitawaambia huyo ni nani, ----- ni bahati mbaya sana kwenu kama mnayo [chapa yake]"? La, huyo si Mungu. Yeye anatuonya juu ya hatari ambayo inaweza kuepukwa. Tunaweza tu kujua kwamba sisi tuko salama mbali na Mnyama huyo kama tunamjua Mnyama huyo ni nani. Tunaweza tu kujua kama sisi tumeondokana na chapa [alama] yake kama tunajua chapa yake ni kitu gani.