>Mwanzo >Soma Vitabu >joka na mwanamke >Joka na mwanamke-Sura ya kwanza >Ni mnyama wa mfano tu

Ni mnyama wa mfano tu

NI MNYAMA WA MFANO TU

 

 Je, yawezekana kujua Chapa [Alama] ya Mnyama huyo ni kitu gani? Twaweza kujua, pasipo kukosea, na ni lazima tujue. Lakini, yatupasa kwanza kuelewa kitambulisho cha Mnyama huyo wa unabii. Hebu na tuweke msingi kwamba Mnyama huyo wa ajabu mwenye tabia kadhaa asichukuliwe kama ni mnyama halisi. Hakuna aliyemwona mnyama aliye na mwili wa chui, kinywa cha simba, na miguu ya dubu. Vitabu vya unabii vya Biblia vinatumia MIFANO na ALAMA (ISHARA). Mnyama huyo anawakilisha kitu fulani. Lakini, je! yeye anawakilisha ishara ya kitu gani hasa? Hapa hatutakiwi kubahatisha. Biblia haiachi mwanya wo wote wa kuwa na mashaka [juu ya jambo hili]. Biblia inajifafanua yenyewe kama komentari ya Mbinguni, nayo inatupatia ufunguo wa kuuelewa unabii wote.

 Katika maelezo ya Biblia kuhusu Mnyama huyo kila kitu chake kimewekwa katika mifano. Kwa mfano, fikiria yale maji anamotoka Mnyama huyo. Yanawakilisha nini? Soma jibu katika Ufunuo 17:15, "Kisha akaniambia, Yale MAJI uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni JAMAA na MAKUTANO na MATAIFA na LUGHA." Hakuna uwezekano wa kulikwepa suala hili la msingi juu ya jambo hili. Mungu alieleza kwa wazi maana ya maji katika [lugha ya] unabii. Mara tu mfano mmoja unapotafsiriwa katika unabii uwao wote ule, basi, KANUNI hiyo hutumika katika kila unabii mwingineo. Maji daima yatakuwa mfano wa watu katika lugha hii ya mafumbo ya unabii wa Biblia.

 Sasa, namna gani juu ya sehemu nyingine za Mnyama huyo wa ajabu wa kitabu cha Ufunuo? Je, zinawakilisha kitu gani? Ili kumjua Mnyama huyo, yatupasa kurudi nyuma kwenye kitabu kile cha Agano la Kale cha Danieli na kulinganisha Maandiko kwa Maandiko [mengine]. Vitabu vya Danieli na Ufunuo kila kimoja kinakifafanua kingine. Vinapatana kabisa kama mkono na glavu [mpira wa kuvaa mkononi] yake. Zingatia, tafadhali, ya kwamba Danieli alikuwa na maono yanayofanana na yale ya Yohana. Hayo yameelezwa katika Danieli 7:2,3: "Danieli akanena, akisema, Naliona katika maono yangu wakati wa usiku; na tazama, hizo pepo nne za mbinguni zilivuma kwa nguvu juu ya bahari kubwa. Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa aina mbalimbali." Aliyaona maji yale ya unabii kama vile Yohana alivyoyaona, ila Danieli aliwaona wanyama wanne wakitoka baharini [maji mengi] badala ya mmoja tu.

 Tumekwisha kuona tayari ya kwamba maji ni mfano wa watu [jamaa] au makutano, lakini, je! wanyama hao wanawakilisha nini? Jibu linapatikana katika fungu la 17, "WANYAMA hao wakubwa walio wanne ni WAFALME wanne watakaotokea duniani." Angalia! Maelezo ni ya wazi kabisa hata hakuna ye yote anayeweza kuuliza swali au kuona mashaka! Mungu anasema kwamba WANYAMA katika unabii wanayawakilisha MATAIFA. Kama vile sisi tulivyo na TAI wa Kimarekani (American Eagle), na Warusi walivyo na DUBU katika msamiati wa kisasa wa masuala ya KISIASA [Tanzania tunaye TWIGA], Mungu naye aliwatumia wanyama zamani, zamani sana kuziwakilisha nchi. Basi, ili kuwa wazi zaidi, Mungu aliongeza maneno haya katika fungu la 23; "Huyo mnyama wa nne atakuwa ni UFALME wa nne juu ya dunia." Kama mnyama yule wa nne anaiwakilisha dola ile ya nne ya historia, basi, wale watatu wa kwanza wangepaswa kuziwakilisha dola zile za kwanza tatu.

Maelezo haya yanarahisishwa zaidi na kueleweka tunapokumbuka kwamba kumekuwa na dola nne tu zilizotawala dunia yote katika historia yote ya dunia hii. Mara kwa mara falme hizo zinatajwa katika unabii wa Biblia na zinatajwa kwa majina yao hasa katika baadhi ya unabii unaohusika katika kitabu cha Danieli. Angalia Danieli 8:20,21 na Danieli 11:2, kama mifano ya maelezo hayo. Katika sura ya pili ya Danieli falme zile zile nne za dunia zinaonyeshwa kwa mfano wa madini nne katika sanamu ile kubwa aliyoiota [Mfalme] Nebukadreza. Dola hizo nne ni BABELI, UMEDI-UAJEMI, UYUNANI na RUMI.